Dar es Salaam. Hapo jana ilitimia miaka mitano rasmi tangu Zuchu alipoachia video ya wimbo wenye heshima kubwa kwake, Sukari (2021) ambao umetayarishwa na Trone na Laizer Classic, mtayarishaji rasmi wa WCB Wasafi.

Kwa Zuchu, Sukari ni wimbo wa mapenzi unaoelezea jinsi upendo wa kweli ulivyo mtamu kama Sukari kiasi kwamba huwezi kamwe kushiba au kutosheka nao.

Humu anaeleza hisia za kumpenda mtu kupita kiasi hadi anahisi maisha yanakuwa mazuri na matamu zaidi akiwa naye akifurahia kupendwa na kumpenda bila masharti.

Wimbo huo wenye mahadhi ya Afro Pop, video yake ilitoka Januari 30, 2021 ikiongozwa na Director Kenny wakati huo akifanya kazi chini ya kampuni ya Zoom Extra, zamani Zoom Production.

Ilipotoka tu ilipokelewa kwa mikono miwili na mashabiki ikitazamwa mara milioni 1 YouTube ndani ya saa 22 na kumfanya Zuchu kuandika rekodi kama msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufanya hivyo.

Hadi sasa video hiyo imetazamwa (views) zaidi ya mara milioni 118.1, na kupokea maoni (comments) 22,000 ambayo yanaijadili huku mengi yakiwa anampongeza Zuchu kwa kazi nzuri yenye ubunifu.

Kwa mwaka 2021, hii ndio ilikuwa video ya muziki iliyofanya vizuri zaidi YouTube ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara ikitazamwa mara milioni 60, ukiwa ni wimbo wa kwanza Bongofleva kufanya hivyo.

Ilifuatiwa na ile ya wimbo wa Wizkid na Tems ambao ulikuja kuchaguliwa kuwania tuzo za Grammy, Essence (2021) iliyotazamwa mara milioni 53, na kwa sasa ikiwa imefikisha milioni 241.3.  

Hata hivyo, kwa mwaka 2022, Zuchu alishindwa kuitetea rekodi yake na kuchukuliwa na mkali wa Afrobeats kutokea Nigeria, Rema kupitia wimbo wake ‘Calm Down’ ambao video yake ilitazamwa mara milioni 300.

Kwa mwaka huo, video ya Zuchu iliyofanya vizuri zaidi YouTube ni ya wimbo, Kwikwi (2020) ambayo ilitazamwa mara milioni 17, kisha ikifuatia na video ya wimbo ‘Mwambieni’ iliyofikisha milioni 14.

Machi 2024, Sukari ikaweka rekodi kama wimbo wa kwanza kutoka kwa msanii solo (aliyeimba peke yake) Tanzania na Afrika Mashariki kwa video yake kutazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube.

Kabla ya Sukari, video za nyimbo zote zilizokuwa zimetazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube, ni zile ambazo walishirikiana wasanii kuanzisha wawili, yaani kolabo.
Nyimbo hizo ni Yope Remix (2019), Inama (2019) na Waah! (2020) zake Diamond Platnumz, na Kwangwaru (2018) yake Harmonize, mwanzilishi wa Konde Music Worldwide.

Mbali na hayo, pia kufanya vizuri kwa wimbo ‘Sukari’ kulichangia Zuchu kuchaguliwa kuwania tuzo za MTV Europe Music Awards (EMAs) 2022 akiwekwa kipengele cha Msanii Bora Afrika.

Washindani wake walikuwa ni Ayra Star (Nigeria), Black Sherif (Ghana), Tems (Nigeria) Musa Keys (Afrika Kusini) na Burna Boy (Nigeria) ambaye alikuja kuibuka mshindi.

Utakumbuka tuzo za MTV EMAs ambazo huandaliwa barani Ulaya na kampuni ya Paramount International Networks, ni moja tuzo kubwa duniani zikiwa na lengo la kutambua mchango wa wasanii na muziki.

Ikiwa imetimia miaka mitano tangu Zuchu kuachia wimbo huo Sukari (2021), hadi sasa hakuna wimbo wake mwingine uliokuja kufikia rekodi zote hapo juu licha ya kutoa kazi nyingi ambazo zimebamba pia.

Ni wazi kuwa baadhi ya mashabiki wake wanajiuliza ni lini Zuchu atawapatia tena wimbo mwingine utakaotikisa kama ‘Sukari’ na kuwafanya kutembelea vifua mbele barani Afrika.

Ikumbukwe Sukari ni wimbo uliotoka takribani miezi 10 tangu Zuchu kutambulishwa WCB Wasafi akiwa ni msanii wa pili wa kike ndani ya lebo hiyo baada ya Queen Darleen.

Umaarufu wake ulikuja kupitia Extended Playlist (EP) yake, I Am Zuchu (2020) iliyofanya vizuri hadi kumuwezesha kushinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kama Msanii Bora Chupukizi.

Miaka mitatu iliyopita, Meneja wa WCB Wasafi, Sallam SK alisema Zuchu anatumbuiza kwa dau la Dola20,000, wastani wa Sh50 milioni kwa show za kimataifa.

Tayari Zuchu amepanda katika majukwaa makubwa ya kimataifa kama Africa Day Concert iliyoandalia na kituo cha MTV Base Africa huko Johannesburg, Afrika Kusini.

Pia ametumbuiza tuzo za All Africa Music Awards (AFRIMA) 2021 – Lagos, Nigeria, AFRIMMA 2022 – Dallas, Texas, Marekani, Sounds City MVP Awards 2023 – Lagos, Nigeria, Trace Awards 2023 – Kigali, Rwanda n.k.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *