Marekani. Mwimbaji maarufu wa Latin Music, Marc Anthony, 57, anatarajia kupata mtoto wake wa nane, na wa pili katika ndoa yake na Nadia Ferreira, 26, ambaye aliwahi kuwa Miss Universe Paraguay.

Marc, mkali wa kibao, You Sang To Me (1999), ametangaza kuwa mkewe ni mjamzito wakati wakihadhimisha miaka mitatu ya ndoa yao iliyofungwa Januari 28, 2023 huko Florida, Marekani.

“Heri ya kumbukizi ya miaka mitatu ya ndoa, ni zawadi kubwa sana ambayo maisha imetupa. Mungu ni mkuu, mtoto wetu Marquito anaenda kuwa kaka mkubwa,” wameeleza katika ujumbe wa pamoja Instagram.

Mtoto wao wa kwanza Marquito alizaliwa Juni 2023, miezi michache baada ya wao kufunga ndoa kwenye jumba la makumbusho la Perez huku mastaa kibao wakihudhuria.

Kati ya mastaa waliofika katika tukio hilo ni pamoja na David Beckham na mkewe, Victoria, Salma Hayek, Lin Manuel Miranda, Luis Fonsi, Romeo Santos na Maluma, mwanamuziki wa Colombia.

Tetesi za wawili hao kuwa pamoja zilianza kufuatia matembezi yao huko Mexico City mnamo Machi 2022 na walithibitisha uhusiano wao kupitia Instagram kwa kuposti picha ya selfie waliyopigwa kwenye ndege.  

Walitangaza kuchumbiana kwao Mei 2022, wakati wa sherehe katika mgahawa wa Sexy Fish huko Florida, huku Ferreira akionyesha picha ya pete ya almasi aliyovishwa kwenye Insta Story yake.

Hadi sasa Marc amefunga ndoa nne na kujaliwa kupata watoto watano, huku wengine wawili akiwapata kati ya mwaka 1994 na 1995 kabla ya kufunga ndoa yoyote maishani mwake.

Alifunga ndoa na aliyekuwa Miss Universe 1993, Dayanara Torres kutokea Mexico hapo Mei 9, 2000, huko Las Vegas, Marekani na kujaaliwa watoto wawili, Cristian Marcus (2001) na Ryan Adrian (2003).

Hata hivyo, ndoa hiyo ilikuja kuvunjika Oktoba 2003, huku Dayanara akiomba talaka hapo Januari 2004. Ili kumsaidia kupona maumivu ya talaka hiyo, Dayanara alibadilisha pete yake ya ndoa na saa aina ya Cartier.

Baadaye Marc alikuja kumuoa mwanamuziki na mwigizaji, Jennifer Lopez (J.Lo) ambaye walishirikiana kwenye muziki kwa kutumbuiza pamoja na kuigiza katika filamu, El Cantante (2006).

Walifunga ndoa Juni 5, 2004, na kufikia Februari 22, 2008 wakajaliwa kupata watoto pacha, Emme Maribel na Maximilian David ambao sasa wanaishi na mama yao.

Baada ya mafanikio katika ndoa na biashara, Aprili 9, 2012, Marc na J.Lo walitangaza kutengana. Marc aliwasilisha kesi ya talaka yao iliyokamilishwa Juni 16, 2014. Na Hadi sasa hii ndio ndoa ya Marc iliyodumu muda mrefu zaidi.

Kufikia Novemba 11, 2014, huko La Romana, Jamhuri ya Dominika, Marc akafunga ndoa yake ya tatu na mwanamitindo Shannon De Lima kutokea nchini Venezuela.

Ila walitangaza kuachana mnamo Novemba 2016, na kumalisha mchakato wa talaka yao hapo Februari 13, 2017, huku wakiwa hajafanikiwa kupata mtoto katika kipindi cha miaka mitatu ya ndoa yao.

Na sasa Anthony Marc, mwanamuziki aliyevuma na kibao chake, I Need You (2002), ametulia katika ndoa yake ya nne na Nadia, Miss Universe 2021.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *