Watu wasiopungua 200 wameaga dunia mapema wiki hii wakati mvua kubwa iliposababisha mfululizo wa maporomoko ya udongo katika mgodi wa madini ya koltani ulioko Rubaya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, eneo ambalo tangu mwaka 2024 liko chini ya udhibiti wa kundi la waasi la M23.

Akisimulia kilichotokea, Franck Bolingo ambaye ni mchimba migodi amesema: “ilinyesha mvua, ikafuatiwa na maporomoko ya udongo ambayo yaliwasomba watu. Baadhi yao walimezwa, wengine walifariki wakiwa kwenye visima. Wengi wangali wamekwama ndani”.

Msemaji wa gavana aliyeteuliwa na waasi katika jimbo la Kivu Kaskazini, Lumumba Kambere Muyisa amesema, waathiriwa ni pamoja na “wachimbaji madini, watoto na wanawake wanaofanya kazi sokoni”.

Ameongeza kuwa watu wasiopungua 20 waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu, baadhi yao katika vituo vya afya vya karibu, na wengine wamehamishiwa Goma, mji wa karibu zaidi ulioko yapata kilomita 50 kutoka eneo la tukio.

Huku shughuli za utafutaji na uokozi zikiwa zinaendelea, maafisa wanasema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka.

Muyisa amesema, gavana wa mji huo amesimamisha kwa muda uchimbaji madini wa kienyeji kwenye eneo hilo na kuagiza kuhamishwa wakazi waliokuwa wamejenga makazi yao karibu na mgodi huo.

Rubaya hutoa karibu asilimia 15 ya koltani yote inayochimbwa duniani ambayo husindikwa kuwa chuma kigumu kinachotumika hasa katika utengenezaji wa simu erevu, kompyuta, na injini za ndege.

Umoja wa Mataifa unasema waasi wa M23 wameupora utajiri wa mgodi huo ili kusaidia kufadhili harakati zake za uasi…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *