Khamenei ametoa matamshi hayo alipohutubia umati wa watu kwenye makaazi yake mjini Tehran kuadhimisha kuanza kwa siku kadhaa za sherehe za miaka 47 ya mapinduzi ya kiislamu ya nchi hiyo yaliyotokea mwaka 1979.
Katika sehemu ya hotuba yake, kiongozi huyo wa mkuu, alisema Marekani inayakodolea macho mafuta, hazina ya gesi na rasilimali nyingine za Iran, na kutahadhrisha kwamba wanataka “kuichukua nchi hiyo, kama walivyowahi kuidhibiti” miaka iliyopita.
“Wamarekani ni sharti wafahamu kwamba wakianzisha vita safari hii, itakuwa vita vya kanda nzima,” amesema Khamenei.
Kiongozi huyo waIran aliongeza pia: “Sisi siyo wachokozi, hatutomtendea ubaya yeyote, hatuna mpango wa kuishambulia nchi nyingine, Lakini iwapo yupo atakayeonesha tamaa na kutaka kutushambulia au kutughasi, Iran itatoa pigo kali kwao.”
Je, Marekani itachukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran?
Matamshi yake yanakoleza moto wa mivutano katika wakati Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu kwa ukandamizaji wake ilioufanya ilipotumia nguvu kuzima maandamano makubwa ya nchi nzima yaliyoitikisa Iran mwezi Januari.
Hii ni mara ya kwanza kwa Khamenei kutoa kitisho cha moja kwa moja tangu Marekani ilipotuma manuari yake ya kijeshi na msafara mkubwa wa meli za kivita kwenye bahari ya Arabia, jirani kabisa na Iran.
Trump amesema anatafakari hatua za kuchukua kuiadhibu Iran kwa “kuwaua waandamanaji.”
Haijafahamika hadi sasa iwapo Trump atatumia nguvu za kijeshi.
Ameitaka mara kadhaa nchi hiyokurudi kwenye meza ya mazungumzo kutafuza makubaliano kuhusu mradi wake wa nyuklia, changamoto nyingine katika mahusiano kati ya Tehran na Washington ambayo hadi sasa haijatatuliwa.
Khamenei asema maandamano yalikuwa sawa na “mapinduzi”
Khamenei pia alionesha kuchukua msimamo mkali dhidi ya maandamano yaliyoigubika nchi hiyo licha ya hapo kabla kukiri kuwa kulikuwa na madai ya msingi ya waandamanaji kuhusu hali ya uchumi.
Maandamano ya umma yalianza Disemba 28, 2025, yakichochewa na kuanguka kwa thamani ya sarafu ya Iran. Baada yalishika kasi na kugeuka kuwa upinzani dhidi ya utawala wa Khamenei.
“Uchochezi wa hivi karibuni ulikuwa sawa na mapinduzi. Lakini bila shaka, mapinduzi hayo yalizimwa,” amesema.
“Lengo lao lilikuwa ni kuharibu maeneo yote muhimu yanayohusisha kuongoza nchi, na kwa sababu hiyo walishambulia vituo vya polisi, majengo ya serikali, kambi za jeshi, mabenki na misikiti– na kuchoma nakala za Quran tukufu. Walivilenga vituo vinavyoendesha nchi.”
Shirika linalofuatilia haki za binadamu nchini Iran lenye makao yake nchini Marekani limeripoti kwamba zaidi ya watu 49,500 wamekamatwa katika ukandamizaji uliofanywa na mamlaka dhidi ya maandamano.
Pia limesema zaidi ya watu 6,714 wameuawa, wengi wao wakiwa waandamanaji.
Takwimu hizo hata hivyo zinakinzana na zile zilizotolewa na serikali ambazo zimeitaja idadi ya watu kuwa 3,117, ikisema 2,427 ni raia na vikosi vya usalama, na kuwataja waliosalia kuwa “magaidi”.