Dar es Salaam. Imesalia miezi michache kabla ya staa wa Bongofleva, Faustina Mfinang maarufu Nandy (33), kutimiza miaka 10 tangu alipotoka kimuziki kupitia wimbo wake, Nagusagusa (2016), uliotayarishwa na Emma The Boy chini ya THT.
Video ya wimbo huo ambayo iliongozwa na Director Hanscana ilitoka Julai 22, 2016 ikiwa ni takribani miezi minne tangu Nandy kushika nafasi ya pili katika shindano la kwanza la karaoke Afrika, Tecno Own The Stage.
Katika shindalo hilo ambalo fainali yake ilifanyika Nigeria, Nandy alizawadia kitita cha Dola15,000 (takriban Sh37.4 milioni) kwa sasa na pia alipewa nafasi ya kupata mafunzo chini ya lebo ya Chocolate City.
Baada ya kurejea Bongo alijiunga na Tanzania House of Talent (THT) ili kunoa zaidi kipaji chake, na punde tu mfululizo wa nyimbo kali kutoka kwake ukachukua nafasi na kumfanya kuwa mwimbaji maarufu.
Ukiachana na Nagusagusa (2016), nyimbo nyingine zilizopaisha jina la Nandy kwa wakati huo, ni One Day (2016), Wasikudanganye (2017), Kivuruge (2017), Ninogeshe (2018) na kadhalika.
Kufanya vizuri kwa nyimbo hizo kulimfanya achaguliwe kuwakilisha nchi katika mradi wa Coke Studio Africa 2017, ambako alifanya shoo ya kuvutia akishirikiana na mwimbaji kutoka Ethiopia, Betty G. Licha ya kuwa msanii mchanga katika Coke Studio, ilikuwa ni fursa kwake kukua akipanda jukwaa hilo lenye hadhi huku akijenga ukaribu na wasanii wenye majina makubwa.
Novemba 2017, Nandy alishinda tuzo ya kwanza ikiwa ni All Africa Music Awards (AFRIMA), hafla iliyofanyika Lagos, Nigeria ambako alitakata katika kipengele cha Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki. Hiyo ni baada ya kuwabwaga Vanessa Mdee, Feza Kessy na Lady Jaydee wote kutoka Tanzania. Wengine walikuwa ni Juliana Kanyomozi kutoka Uganda na Victoria Kimani wa Kenya.
Ushindi huo ulimfungulia milango ya kutambulika kitaifa na kupata mikataba ya matangazo ya kibiashara. Mathalani alikuwa balozi katika kampeni ya kitaifa ya afya na usafi wa mazingira. Alishinda tuzo nyingine kama AMI Awards Africa 2018, Africa Entertainment Awards, USA (AEAUSA) 2021, African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2021 na The Orange Awards 2023.
Kubwa zaidi ni Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) ambazo ameshinda mara nne vikiwemo vipengele vyenye heshima kama Msanii Bora wa Kike wa Mwaka na Msanii Bora wa Kike Bongofleva. Ni wazi kuwa kushinda ni matokeo ya kufanya vizuri kwa nyimbo zake na pia albamu, The African Princess (2018), pamoja na Extended Playlist (EP) zake tatu Taste (2021), Wanibariki (2021) na Maturity (2022).
Alikuja kufungua lebo yake inayokwenda kwa jina sawa na la albamu yake ya kwanza. Lebo hiyo ndio ilimtambulisha Yammi katika Bongofleva kupitia EP yake Three Hearts (2023) yenye nyimbo tatu.
Chini ya The African Princess Label, Yammi akawa mwanamuziki maarufu akitamba na nyimbo zake kama Namchukia (2023), Tiririka (2023), Nitadumu Nae (2024), Kukupenda (2024) na kadhalika. Hadi anaondoka katika lebo hiyo Mei 2025, Yammi tayari alikuwa mwanamuziki maarufu huku akiwa ameshirikiana na Nandy katika wimbo mmoja, Lonely (2024) uliotayarishwa Mafeeling Records.
Yammi ameingia katika orodha ya waimbaji wa kike Bongo ambao Nandy ameshirikiana nao, wengine ni Lulu Diva, Mtaalamu (2023), Mimi Mars, Pole (2024), Maua Sama, Poa (2024) na kadhalika. Akiwa kwenye tamasha la Fiesta 2016, Nandy akajikuta akipendana na staa mwenzake Billnass ambaye ndiye msanii aliyeshirikiana naye mara nyingi zaidi katika muziki kwa muda wote.
Wawili hao waliitwa katika tamasha hilo na kupangiwa kutumbuiza Sumbawaga, lakini wakaenda kulala Mbeya na huko ndipo uhusiano ulianzia hadi walipokuja kufunga ndoa Julai 2022 na sasa wana mtoto mmoja. Hadi sasa Nandy na mumewe Billnass wametoa nyimbo tano pamoja ambazo ni Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021), Bye (2022) na Totorimi (2024). Wakati Nandy akiwa mjamzito, aliachia video ya wimbo wake, Napona (2022) akimshirikisha Oxlade kutoka Nigeria na katika video hiyo Billnass ametokea ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo.
Katika toleo la awali la video yao (visualiser), Totorimi (2024), Nandy na Billnass wameonyesha jumba la kisasa na la kifahari ambalo linathibitisha wao ni mastaa wanaojua kuzisaka fedha. Ili kuvutia zaidi biashara ya muziki alianzisha tamasha ‘Nandy Festival’ alilolingoza kwa mafanikio kwa misimu kadhaa kabla ya kusimama ghafla 2022.
Kwa sasa akisimama kama chapa (brand), Nandy anaendelea kutumia umaarufu wake ulioletwa na muziki kufanya biashara nyingine. Alishaingiza sokoni bidhaa za vipodozi na pia anapangisha nyumba za makazi ya muda.