
Dodoma. Serikali imesema kuwa wakandarasi wa ujenzi wa barabara kutoka Tanganyika hadi Uvinza wamesharudi kwenye maeneo yao.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumatatu Februari 2, 2026 na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya ambaye ameeleza kulikuwa na changamoto kidogo kwenye utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo.
Kasekenya ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Janeth Pinda ambaye ameuliza Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Wilaya ya Tanganyika hadi Uvinza.
Katika swali la nyongeza mbunge huyo amehoji ni sababu zipi zilipelekea wakandarasi hao kuondoka katika maeneo ya utekelezaji wa miradi yao, hali iliyosababisha kazi ya ujenzi kusimama.
Pinda amesema kujengwa kwa vipande vipande katika barabara hiyo ni moja ya chanzo cha kusua sua kwa mwendelezo katika ujenzi wa barabara hiyo muhimu.
“Mheshimiwa Naibu Spika (Daniel Sillo), ujenzi wa barabara hii unatekelezwa kwa awamu ambapo ujenzi kwa sehemu ya kwanza ya Mpanda – Vikonge (kilometa 37.65) umekamilika.
“Ujenzi wa sehemu ya pili ya Vikonge – Luhafwe (kilometa 25) unaendelea na umefikia asilimia 70,” amesema Kasekenya.
Naibu Waziri ametaja ujenzi wa sehemu ya tatu ya Luhafwe – Mishamo/Butamata (kilometa 37.35) kwamba unaendelea na umefikia asilimia 30.6.
Amesema kwa sehemu iliyobaki ya Mishamo – Uvinza (kilometa 95.6), Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi.