Nazma Khan, mwanzilishi wa “Siku ya Hijabu Duniani”, ameiambia televisheni ya Al Jazeera ya Qatar kwamba chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi haiishii tena katika vitendo vya ukatili au uonevu, bali imechukua sura hatari zaidi ya kunyamazisha sauti za wanawake Waislamu kwa jina la kutetea haki zao.

Akizungumza kwa mnasaba wa “Siku ya Hijabu Duniani” ambayo huadhimishwa Februari 1, Nazma Khan ameongeza kwamba “wale wanaozungumza kwa niaba ya haki za wanawake na kusema kwamba wanataka kuwakomboa wanawake Waislamu ndio wale wale wanaonyamazisha sauti zetu,” akisisitiza kwamba matamshi haya yanazalisha ubaguzi katika sura mpya, inalokubalika zaidi katika anga ya umma.

Amesema, kunyamazisha huko kwa sauti ya Wanawake Waislamu huanza katika hatua za mwanzo za kielimu, akieleza kuwa ubaguzi dhidi ya wanafunzi Waislamu umeongezeka sana.

Mwanaharakati huyo, Mwislamu wa Marekani mwenye asili ya Bangladesh, ameelezea kwamba “tafiti zinaonyesha kuwa kiwango cha uonevu nchini Marekani ni takriban 20% kwa ujumla, lakini kinafikia 60% kwa wanafunzi Waislamu, ambacho ni mara 3 zaidi,” akisisitiza kwamba jambo hili lazima libadilike.

Nazma Khan anaamini kwamba kukabiliana na dhana potofu si utetezi katika maneno tu, bali pia kufungua nafasi za uelewa wa moja kwa moja, jambo ambalo lilimchochea kufikiria mpango unaowataka wanawake, bila kujali dini zao, kuvaa hijabu kwa siku moja.

Amesema: “Labda kwa njia hii watu wataelewa kwamba vazi la hijabu si kama vyombo vya habari vinavyoielezea. Hatufichi mabomu au kupanga kulipua chochote.”

Nazma Khan

Kwa mujibu wa Nazma Khan, athari muhimu zaidi ya mpango huo ni mabadiliko ya taratibu katika mijadala ya umma, kwani shule, vyuo vikuu, maeneo ya kazi na hata baadhi ya taasisi za kisiasa sasa zinashiriki katika kuadhimisha Siku ya Hijabu Duniani, iliyochangia “kubadilisha simulizi ambayo imekuwa ikihusishwa na wanawake Waislamu kila wakati.”

Licha ya haya, anasema gharama anayolipa kwa msimamo huo bado ni kubwa, kwani anapokea vitisho na barua za chuki kutoka sehemu mbalimbali za dunia zikimlenga yeye na familia yake, lakini anasisitiza kwamba kurudi nyuma si chaguo. “Inatisha,” anasema, “lakini hatuwezi kuacha msimamo wetu. Lazima tuwe jasiri kwa sababu sisi ni wanawake Waislamu.”

Nazma Khan amemalizia ujumbe wake kwa kusema kwamba wanawake wa Kiislamu hawahitaji mtu yeyote kuzungumza kwa niaba yao, akisisitiza: “Hatuhitaji mzungu kutukomboa. Tunaweza kujikomboa. Tunachoomba ni kuruhusiwa kuzungumza na kusikilizwa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *