Refa mwenye historia ya bahati na klabu za Kaskazini mwa Afrika pindi zinapocheza nyumbani kwenye mashindano ya Klabu Afrika, Tom Abongile kutoka Afrika Kusini, amepangwa kuchezesha mechi ya kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baina ya FAR Rabat na Yanga itakayochezwa Februari 7, 2026.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Abongile (34) kuchezesha mechi hiyo ikiwa ni ya pili kwake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya ile baina ya Esperance na Stade Malien.
Timu za Kaskazini mwa Afrika ambako lugha kuu inayozungumzwa ni Kiarabu, zimekuwa na bahati kubwa ya kutopoteza nyumbani pindi Abongile anapochezesha mechi.
Refa, Tom Abongile kutoka Afrika Kusini, ambaye amepangwa kuchezesha mechi ya kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya FAR Rabat na Yanga itakayochezwa Februari 7, 2026.
Mchezo baina ya Esperance na Stade Malien ambao amechezesha mwaka huu, ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Msimu uliopita, refa huyo alichezesha mechi nne za mashindano ya Klabu Afrika ambazo zilichezwa Kaskazini mwa Afrika na wenyeji waliibuka na ushindi pasipo kuruhusu nyavu zao kutikiswa.
Abongile kiujumla amechezesha idadi ya michezo 12 ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ametoa idadi ya kadi 57 za njano na kadi moja nyekundu.
Refa, Messie Mvouutou kutoka Congo, ndiye aliyechaguliwa kuchezesha mechi kati ya Azam na Maniema ya DR Congo katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar Jumamosi, Februari 7. Picha na Mtandao
Mkongo kuichezesha Azam na Wakongo
Mchezo unaofuata wa Azam na Maniema ya DR Congo katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar Jumamosi, Februari 7 utachezeshwa na Refa, Messie Mvouutou kutoka Congo.
Styven Moyo na Malondi Yanes watakuwa wasaidizi huku Ruth Bilembi akiwa Refa wa akiba wote wakiwa wanatoka Congo.
Kwa upande mwingine, mchezo baina ya Singida Black Stars na CR Belouizdad, Jumapili Februari 8, 2026 utachezeshwa na Refa Adalbert Diouf kutoka Senegal.