
Dar es Salaam. Siku mbili baada ya matumaini ya Simba kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kuzikwa rasmi, Meneja Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally amewataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu.
Sare ya mabao 2-2 ambayo Simba ilipata nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi Jumapili, iliifanya imalize raundi nne za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ikiwa na pointi moja ambayo haitoshi kuifanya iingie robo fainali.
Ahmed Ally amewaomba mashabiki wa timu hiyo kutovunjika moyo na kilichoikumba timu yao katika Ligi ya Mabingwa Afrika na badala yake kiwe chachu ya kufanya vyema zaidi.
“Tusife moyo wala tusiingie unyonge ndugu zangu Wana Simba. Kushindwa kufanya vizurii kimataifa msimu huu isitunyong’onyeshe bali itupe nguvu ya kujipanga msimu ujao.
“Wakati mwingine ili ufike juu lazima uanzie chini, Msimu huu tumeteleza lakini tusiivunjie adabu timu yetu ambayo imetupa heshima kubwa Afrika.
“Nafahamu wasiotutakia mema watajaribu kunadi kufeli kwetu msimu huu kuwa ni tatizo kubwa ambalo halijawahi kutokea duniani lengo ni kuchonganisha mashabiki na timu yao mashabiki na viongozi wao,” amesema Ally.
Ally amesema mashabiki wa Simba wanapaswa kuwa kitu kimoja na anaamini kuna mambo mazuri yanakuja kwa timu yao.
“Wakati huu tuchague cha kusikiliza na tuchague cha kuongea. Wengi wanaonekana kama wanaipigania klabu au wanatutetea lakini uhalisia wanachochea vurugu klabuni kwetu
“Tuilinde nembo ya klabu yetu.. Mnyama atarejea tuu kwenye ufalme wake tena hivi punde tu,” amesema Ahmed Ally.
Baada ya kushindwa kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba sasa imebakiza matumaini katika Ligi Kuu ambako inashika nafasi ya sita kwenye msimamo ikiwa na pointi 16 na pia Kombe la Shirikisho la CRDB.