Dar es Salaam. Kuna matukio ndiyo basi tena, yamebaki stori tu za vijiweni. Umewahi kujiuliza wale rafiki zao uliosoma nao shule ya msingi wako wapi? Je bado mnawasiliana au mlitemana siku ya mahafali?

Watu wengi hujikuta wakipunguza idadi ya watu kila wanavyotoka hatua moja kwenda nyingine. Hili siyo jambo la kushangaza kwani machaguo ya binadamu hubadilika kulingana na wakati.

Ingawa wapo baadhi ya watu ambao huendelea kuwa na mawasiliano hata baada umbali lakini ni wachache mno. Acha tuseme kwenye hii ‘Darasa la Saba’ Mbosso ameweza kuwarudisha mashabiki wake utotoni.

Hisia mchanganyiko na kumbukumbu za kufurahisha, zinajionesha kwenye simulizi na shuhuda za mashabiki wake anazochapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Wapo wanaosimulia kwa hisia namna walivyoishi na rafiki zao wa shule ya msingi. Bila kusahau mtindo wa mapacha wanaosimulia mikasa waliyokutana nayo shule ya msingi kutokana na kufanana kwao.

Aidha wimbo huo umeonesha, watu huwa na ndoto nyingi sana wanapokuwa shule ya msingi. Lakini kadri muda unavyozidi kwenda mambo yanabadilika.Pia ameonesha siyo wote wanaoshindwa kumaliza masomo ni wazembe wakati mwingine maisha yanawalazimu.

Akizungumzia wimbo wake, Mbosso alisema hajalenga mpenzi bali rafiki wa kike shule ya msingi

“Maisha ambayo tuliishi, vijana wanaweza wasisome ila darasa la saba ni mchongo rahisi. Huku sekondari ndiyo huwa mitikasi. Kufika darasa la saba rahisi sana, lengo siyo mchumba ni rafiki. Lakini shule ukiwa na rafiki wa kike ilikuwa unasimulia watu yule ni mchumba wangu, lengo ni kuwaambia watu unaweza ukawa unamkumbuka rafiki yako,”alisema Mbosso

Wimbo huo kupitia mtandao wa YouTube umefanikiwa kutazamwa zaidi ya mara milioni mbili, ndani ya siku sita. Kwa mafanikio haya ya muda mfupi ni wazi kwamba wimbo huu umewagusa wengi

Maoni ya mashabiki

Akizungumzia wimbo huo Warioba Thobias anasema “Mbosso Khan ndiye the best kwenye utungaji wa nyimbo ambazo zinagusa watu. Bro tunakukubali daima,”

Naye Darado Komba, “Nikikumbuka shule ya msingi niliandika barua, halafu nikaibiwa ile barua. Jamaa akaipeleka kwa mkuu. Halafu mkuu alikuwa anasoma mstari mmoja mmoja kila akija darasani,”

Aidha Winnie Sande, “Yani Mbosso nakukubali, hii ngoma imenilenga mazima na umefanikiwa kunikutanisha na ex wangu tuliyeachana shule ya msingi mwaka 2007 takribani miaka 19 iliyopita,”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *