Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrick Soraga, aipongeza Chapa ya Yas na Mixx kutimiza mwaka mmoja, pia amesema kuwa sekta binafsi ni mhimili wa msingi katika kuisukuma Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali, huku akisisitiza ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi kama kielelezo cha maendeleo ya Tehama.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Januari 23, 2026 wakati wa hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu chapa za mawasiliano za Yas na huduma za kifedha za kidijitali za Mixx zilipojitambulisha upya sokoni, Novemba 2024.

“Zanzibar sasa hivi tupo katika safari ya kidigitali na ndio maana tumeona tutafute wadau ambao ni wabobezi katika mambo haya ya Tehama ili tuweze kushirikiana nao. Tunayo mipango mikubwa kuhakikisha Zanzibar inasonga mbele kidigitali,” amesema Waziri Soraga.

Amesisitiza kuwa safari ya kidijitali bado haijakamilika na sekta binafsi ina nafasi ya kipekee kama kiongozi wa mabadiliko hayo, akihimiza uwepo wa wadau zaidi ili Tanzania isonge mbele kwenye uchumi wa kidijitali na maendeleo ya jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Axian Telecom Group, Hassan Jaber amesema tangu kuzinduliwa kwa chapa hizo, lengo lilikuwa ni kujenga jamii jumuishi ya kidijitali na kuunganisha watu zaidi kupitia teknolojia.

“Mwaka mmoja uliopita tulizindua Yas na Mixx tukiwa na ndoto ya kuikuza kizazi cha kidijitali na kuunganisha jamii barani Afrika.

“Leo, tunapoadhimisha mwaka mmoja, ninafurahi kuona ndoto hiyo ikichukua sura halisi.Katika kipindi cha miezi 12, tumeboreshaji mtandao wetu, tumepanua huduma za 5G na Fiber, tumeongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali na kuleta matokeo chanya kwa wateja wetu.

“Maono yetu bado ni yale yale, kuifanya Yas kuwa moja ya chapa imara zaidi barani Afrika, huku tukihakikisha maendeleo yanakuwa jumuishi na yanayochangia malengo ya muda mrefu na mabadiliko ya kidijitali nchini Tanzania,” amesema Jaber.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas- Tanzania, Pierre Canton Bacara, amewashukuru wateja, washirika, wafanyakazi na jamii kwa ujumla kwa kuufanya mwaka wa kwanza kuwa “mwaka wa mageuzi ya kweli “Tunapoadhimisha mwaka mmoja wa Yas, tunawashukuru wote waliotembea nasi katika safari hii. Mwaka huu tumefanya uwekezaji wa zaidi ya Sh1 trilioni katika kupanua na kuboresha mtandao wetu, na kuhakikisha tunawafikia wateja zaidi ya milioni 29.

“Lengo letu ni kuwa mshirika wa kweli wa kidijitali kuwawezesha vijana, wafanyabiashara, mashirika makubwa na hata taasisi za Serikali kufanikiwa katika dunia ambayo kila siku inazidi kukua kidijitali,” amesema.

Mbali na mtandao, Yas imekuwa mstari wa mbele katika miradi ya kijamii-ikiwemo kusaidia wanafunzi kupata vifaa vya kujifunzia kidijitali, kuwajengea uwezo wasichana katika masuala ya teknolojia, ujasiriamali, pamoja na miradi ya kuhifadhi mazingira vijijini na mijini.

Bacara aliongeza kuwa “Huu ni mwanzo tu.

Tunabaki na dhamira ya kupanua huduma, kuongeza ubora wa uzoefu wa kidijitali kwa kila Mtanzania, na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya taifa letu”.

Kupitia kampeni yake ya Anzia Ulipo, Yas imeendelea kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, kuwahamasisha vijana na kuongeza kasi ya ujumuishaji wa kidijitali nchini.

Inapoelekea kwenye mwaka wa pili wa ukuaji, Yas imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika kufikia uchumi wa kidigitali unaotegemea teknolojia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *