Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeidhinisha rasmi zoezi la kuteketezwa kwa nyaraka zilizotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025 baada ya kukamilika kwa muda wa siku 90 tangu kumalizika kwa uchaguzi huo.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha ZEC kilichofanyika Februari pili 2026, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kisheria ya kuhakikisha uchaguzi unakamilika kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo Kwa mujibu wa ZEC.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari makao makuu ya ZEC Maisara, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji George Kazi amesema zoezi hilo linafanyika kwa kuzingatia kifungu cha 98(3) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018, kinachoitaka Tume kuharibu nyaraka zote zinazohusiana na Uchaguzi Mkuu baada ya kupita siku 90 tangu kukamilika kwa uchaguzi husika.
Jaji Kazi ameongeza kuwa kabla ya kuidhinisha utekelezaji wa zoezi hilo ZEC imejiridhisha kutokuwepo kwa amri yoyote ya Mahakama inayozuia utekelezaji wa hatua hiyo.
Aidha, amewahimiza wadau wote wa Uchaguzi kushirikiana ipasavyo katika utekelezaji wa zoezi hilo ili kuhakikisha linafanyika kwa mafanikio, uwazi na kwa kuzingatia kikamilifu misingi ya kisheria na taratibu zilizowekwa.
Mhariri @moseskwindi