Droni ya doria na ya intelijinsia ya vikosi vya ulinzi vya Iran imefanikiwa kukamilisha kwa mafanikio operesheni yake katika maji ya kimataifa huku ripoti zikiarifu kuwa askari wa Marekani wameitungua ndege moja isiyo na rubani sawa na hiyo.

Shirika la habari la Fars imeeleza kuwa kazi ya msingi ya ndege zisizo na rubani za aina hiyo ni kufuatilia harakati zote za kijeshi katika maeneo ya karibu na Jamhuri ya Kiislamu, na kuongeza kuwa data kutoka kwa ndege hizo hupitishwa na kupokelewa na vituo vya ardhini kwa wakati sahihi.

Wakati huo huo chanzo makini kilichozungumza na Shirika la Habari la Tasnim kimeitaja ndege hiyo kuwa ni ndege isiyo na rubani (droni) kwa jina la  Shahed-129. Chanzo hicho makini kimeeleza haya baada ya ripoti kutoka za vyombo vya habari vya lugha ya Kiingereza kudai kuwa ndege ya kivita ya Marekani imeitungua droni ya Iran kutoka kwenye meli ya kubeba ndege ya USS Abraham Lincoln.

Chanzo hicho kimeongeza kuwa: Droni ya Shahed-129 ilikuwa ikitekeleza operesheni yake ya kawaida na ya kisheria ya intelijinsia, ufuatiliaji na kupiga picha katika maji ya kimataifa. Huu ni utaratibu wa kawaida na halali.

Chanzo hicho makini kimeendelea kueleza kuwa mawasiliano, hata hivyo, baadaye yalipotea na uchunguzi unaendelea ili kubaini sababu ya kukatwa mawasiliano na maelezo zaidi yatatolewa mara tu baada ya kukamilika uchunguzi.

Jana Jumanne CENTCOM ilitangaza katika taarifa yake kuwa iliishambulia ndege isiyo na rubani ya Iran ili kuwalinda wanajeshi wake. Taarifa hiyo ilidadi kuwa CENTCOM haina nia ya kushadidisha mivutano na kwamba ilifanya hivyo eti kwa ajili ya kujilinda. 

Matukio haya yanaripotiwa huku Marekani ikiwa imejiimarisha kijeshi katika eneo la Asia Magharibi ikiwemo katika Ghuba ya Uajemi sanjari na vitisho vya mara kwa mara vilivyotolewa na Rais Donald Trump vya kuanzisha uchokozi mpya wa kijeshi dhidi ya Iran.

Jumapili iliyopita Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alionya kwamba vita vya kikanda vitazuka iwapo Marekani itathubutu kushambulia ardhi ya Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *