
Rached Ghannouchi, mkuu wa harakati ya Ennahda na spika wa zamani wa Bunge la Tunisia, alitangaza jana Jumanne kwamba hatakata rufaa mahakamani dhidi ya hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela aliyokatiwa katika kile kinachojulikana katika vyombo vya habari kama “Kesi ya Kula Njama – 2,” akisema kwamba kesi hiyo haina dhamana ya haki.
Haya yamekuja katika taarifa rasmi iliyochapishwa na timu ya utetezi ya Ghannouchi kwenye Facebook, ambapo imesema: “Timu ya utetezi inataka kuufahamisha umma kuhusu uamuzi wa Ghannouchi wa kukataa kutoa maoni kuhusu uamuzi huo, kutokana na imani yake thabiti kwamba hakuna dhamana ya kesi ya haki, na kwamba kesi zinazopelekwa mahakamani ni za kubuni na za kisiasa.”
Timu ya utetezi ya mwanasiasa huyo mkonge wa Tunisia imesisitiza kwamba Rached Ghannouchi hana hatia yoyote ya tuhuma zilizotolewa dhidi yake, ikisisitiza kuwa ataendelea kutetea haki yake ya kusikilizwa kwa uhuru wa kujieleza.
Mahakama ya Rufaa katika mji mkuu, Tunis, iliongeza hukumu dhidi ya Ghannouchi hadi miaka 20 jela. Hukumu kama hiyo pia imetolewa dhidi ya Kamal Badawi, afisa wa zamani wa usalama, na watu wengine 5 wamehukumiwa vifungo tofauti. Hapo awali, Mahakama ya Mwanzo ya Tunisia ilikuwa imewahukumu kifungo cha miaka 14 jela.
Rached Ghannouchi amekuwa jela tangu Aprili 17, 2023, baada ya nyumba yake kuvamiwa na vyombo vya dola kwa madai ya “kufanya uchochezi dhidi ya usalama wa taifa,” na maamuzi kadhaa ya awali yametolewa dhidi yake katika kesi mbalimbali.
Serikali ya Tunisia hapo awali ilidai kwamba wafungwa wote wameshtakiwa kwa makosa ya jinai, ikikana kwamba hakuna yeyote aliyekamatwa kwa sababu za kisiasa. Hata hivyo makundi ya kisiasa nchini humo yanasema hatua za kipekee zilizoanzishwa na Rais Kais Saied mnamo Julai 2021 ni “mapinduzi dhidi ya Katiba na juhudi za kuimarisha utawala wa kidikteta”