Ndani ya siku mia za uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imefanikiwa kuwasha umeme katika kata ya Mlima wa Uluguru, Manispaa ya Morogoro, hatua inayotarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza idadi ya watalii katika eneo hilo.
Akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Ruvuma, Kata ya Mlimani, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amesema uwepo wa umeme utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi, ikiwemo kuanzisha biashara ndogondogo na kuboresha huduma za kijamii.
“Umeme ni chachu ya maendeleo. Wananchi watapata fursa za kuanzisha miradi ya kiuchumi, kuongeza kipato na kuboresha maisha yao kwa ujumla.”
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali, amemwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kuhakikisha miche 1,000 ya karafuu inapelekwa katika eneo hilo ili wananchi waipande kama zao la biashara litakaloongeza kipato chao.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Morogoro, Fikiri Juma, amesema kuwashwa kwa umeme kutawawezesha vijana kubuni na kuendesha biashara mbalimbali, hali itakayosaidia kupunguza tatizo la ajira na kuinua uchumi wa eneo hilo.
Wananchi wa kata ya Mlima wa Uluguru wameipongeza Serikali kwa hatua hiyo, wakisema ni mwanzo wa maendeleo makubwa katika sekta za uchumi na utalii.
Aidha Mhandisi Emmanuel Chamoto Kaimu Meneja Mkoa wa Morogoro Kaskazini amesema pamoja na kufikisha umeme katika kata hiyo ya mlimani lakini eneo la hilo lilikua ni gumu kutokana na uwepo wa milima mikubwa na miundombinu kuifikisha kwa shida huku akishukuru serikali kwa kutoa bajeti zinazowezesha kuteleza miradi ya umeme.
(Feed generated with FetchRSS)