GEITA: HALMASHAURI ya wilaya ya Geita mkoani Geita imefanikiwa kukusanya kiasi cha sh bilioni 6.37 sawa na asilimia 45.42 ya makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani mwaka wa fedha 2025/26.
Aidha halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya na kupokea jumla ya Sh bilioni 51.63 sawa na asilimia 49.84 ya kiasi cha Sh bilioni 102 ambayo ni makisio ya mwaka huu wa fedha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Karia Rajabu ametoa taarifa hiyo katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika makao makuu ya halmashauri yaliyopo kata ya Nzera.

Karia amesema pesa zilizopokelewa kutoka serikali kuu zinahusisha matumizi mbalimbali ikiwemo mishahara, ruzuku ya matumizi mengineyo (OC) pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri ilipanga kutekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya sh bilioni 20.9 kutokana na mapato ya ndani, serikali Kuu na wadau wa maendeleo.
“Hadi kufikia Desemba, 2025, jumla ya Sh bilioni 6.75 zimepokelewa kutoka Serikali Kuu na wadau kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo”, amesema.
Amesema pia halmashauri imehamisha na kutumia sh bilioni 4.76 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika ngazi ya msingi, halmashauri pamoja na usimamizi wa miradi.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Geita, Christopher Kahesi amesisitiza watendaji na madiwani kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Kahesi ameitaka halmashauri kutumia vyema fursa ya biashara ya madini ujenzi kama sehemu ya kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani na kuweza kufikia lengo kwa mwaka huu wa fedha.
Katibu Tawala wa wilaya ya Geita, Lucy Beda amewaomba wabunge, madiwani na watendaji wote wa halmashauri hiyo kutanguliza nidhamu katika utendaji wao wa kila siku kuepuka migogoro.
Amesema iwapo kuna sintofahamu baina ya viongozi ipo haja ya kutumia kwa ufasaha mikutano ya ndani ili kutatua badala ya kuvutana mbele ya hadhara ili kujenga nidhamu ya utumishi.