
Katika taarifa yao iliyotolewa leo New York, Marekani, viongozi hao wa mashirika lile la afya, WHO, Elimu, Sayansi na UTamaduni, UNESCO, Haki za Binadamu, OHCHR, la kuhudumia watoto, UNICEF, la masuala ya wanawake, UN Women, na afya ya uzazi na idadi ya watu UNFPA, wamesema licha ya mafanikio yaliyopatikana, kando ya hao walio hatarini kukeketwa, zaidi ya wasichana na wanawake milioni 230 bado wanaishi na madhara ya kudumu za ukatili huo.
Theluthi mbili ya wakazi wa maeneo yatekelezaji FGM hivi sasa wanapinga kitendo hicho
Viongozi hao wamesema juhudi za kuzuia ukeketaji katika muongo uliopita zimechangia kupungua kwa kiwango cha tatizo hilo, huku takribani theluthi mbili ya watu katika nchi zilizoathirika vibaya, sasa wakionesha kuunga mkono kutokomezwa kwake.
Mikakati iliyothibitishwa kufanya kazi ni pamoja na mipango inayoongozwa na jamii, elimu, ushirikishwaji wa viongozi wa kidini na wa jamii, pamoja na huduma madhubuti za kuwasaidia manusura.
Upungufu wa ufadhili ni ‘mwiba’ kwa mafanikio yaliyopatikana
Hata hivyo, mashirika hayo yameonya kuwa upungufu wa ufadhili na kupungua kwa msaada wa kimataifa kunahatarisha kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mingi. Viongozi wamesema bila ufadhili wa uhakika na unaotabirika, programu nyingi zinaweza kupunguzwa, na hivyo kuwaweka mamilioni zaidi ya wasichana katika hatari.
Dola 1 dhidi ya FGM huleta faida mara 10
Wamebainisha kuwa kila dola moja inayowekezwa inaleta faida mara 10 na wametoa wito kwa serikali na wafadhili kuweka kipaumbele katika kuzuia ukeketaji kupitia jamii na kuhakikisha upatikanaji wa huduma kwa manusura ili kumaliza kabisa ukeketaji.
FGM hugharimu mifumo ya afya dola bilioni 1.4 kila mwaka
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika ujumbe wake wa siku hii yenye maudhui kutokomeza FGM ifikapo mwaka 2030, amesema ni vema kurejelea upya Ahadi ya kulinda haki za wanawake na wasichana kila mahali, na kuhakikisha wanaishi bila ukatili wala hofu.
Amesema, “kwa pamoja, tunaweza kukomesha dhuluma hii mara moja na kwa wote.”
Guterres amekumbusha kuwa kutochukua hatua ni kunaleta gharama kubwa kwani, kutibu madhara yatokanayo na ukeketaji hugharimu takribani dola bilioni 1.4 kila mwaka.