
Mtaalamu wa tiba ya viungo Adam James, amezungumzia baadhi ya harakati na alama za kimwili za Donald Trump na kutahadharisha kwamba, huenda rais huyo wa Marekani asiishi zaidi ya miaka miwili hadi minne tu ijayo.
James, ambaye ana tajiriba ya miaka 14, ametangaza kwenye kipindi cha YouTube cha David Packman kwamba yumkini Trump ana dalili za ugonjwa wa ubongo wa Frontotemporal dementia (FTD), unaoathiri ubongo ikiwemo sehemu yake ya mbele.
Mtaalamu huyo wa tiba ya viungo ametaja baadhi ya alama na harakati za kimwili za rais wa Marekani, ikiwa ni pamoja na utembeaji usio wa kawaida, uzungumzaji usioeleweka, matatizo ya kudhibiti utikisaji wa viungo na makosa ya mara kwa mara anayofanya katika kutoa taarifa za msingi, kama ushahidi unaoweza kuthibitisha suala hilo.
James amebainisha kwamba, ikiwa utambuzi wake kuhusu ugonjwa alionao Trump utakuwa sahihi, yumkini rais huyo wa Marekani akawa amebakisha miaka miwili hadi minne tu ya kuishi.
Ameongezea kwa kusema: “umri mkubwa na hali zilizopo zinaweza kuongeza kasi ya kushradi ugonjwa wa rais wa Marekani.”
Inafaa kuashiria kwamba uvumi kuhusu afya ya Trump ulianza baada ya makamu wake wa rais J.D. Vance kufanya mahojiano na vyombo vya habari na kutangaza utayari wake wa kumrithi Trump iwapo kutatokea “janga baya,” lakini Vance alisisitiza kwamba rais wa Marekani “yuko katika hali nzuri.”
Maoni hayo yalienea haraka kwenye mitandao ya kijamii, na msemo “Trump amekufa” ukasambaa kwenye mitandao duniani.
Halikadhalika, Trump ameonekana katika picha mbalimbali akiwa na michubuko mikononi mwake na uvimbe miguuni, na kuzipa nguvu tetesi zilizopo kuhusu afya yake, licha ya Ikulu ya White House kutangaza kwamba michubuko na uvimbe huo vimetokana na tatizo sugu la uzungukaji wa damu (chronic venous insufficiency)…/