Manchester United imeendeleza kugawa dozi katika Ligi Kuu England (EPL) ikiwa chini ya Meneja wa muda Michael Carrick baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Mabao ya ushindi ya Man United katika mechi ya leo yamepachikwa na Bryan Mbeumo na Bruno Fernandes katika kila kipindi cha mchezo.

Mbeumo aliifungia bao la kuongoza Man United katika dakika ya 38 akimalizia pasi ya Kobbie Mainoo na katika dakika ya 81, Fernandes akafunga la pili akimalizia pasi ya Diogo Dalot.

Bao moja la Mbeumo katika mchezo wa leo linamfanya ajiandikie rekodi ya kufunga bao katika mechi nne mfululizo za Man United katika Ligi Kuu England (EPL).

Matokeo hayo yameifanya Manchester United izidi kuweka hai matumaini yake ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kwa sasa imejichimbia katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 44 ambazo ni nne juu ya Chelsea iliyo katika nafasi ya tano na pointi tano zaidi ya Liverpool iliyopo nafasi ya sita kwenye msimamo.

Na pia wapo nyuma ya Man City iliyopo nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi tatu.

Pia wamevuka rekodi yao mbovu ya msimu uliopita ya kumaliza wakiwa wamevuna idadi ya pointi 42.

Katika mchezo huo wa leo, nahodha wa Spurs, Criatian Romero alionyeshwa kadi nyekundu na refa Michael Oliver katika dakika ya 29 kwa kosa la kumchezea rafu, Casemiro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *