Mwanza. Licha ya kucheza pungufu kwa dakika 52, Azam FC imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB iliyochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo.

Azam wamecheza na idadi ya wachezaji 10 uwanjani kuanzia dakika ya 68 hadi dakika ya 120 baada ya beki wake Yoro Diaby kuonyeshwa kadi nyekundu na Refa Sifu Amon kwa kosa la kumchezea rafu Prince Dube aliyekuwa anaelekea langoni mwake.

Mchezo huo ulilazimika kuchezwa kwa dakika 120 kwa vile muda wa kawaida wa dakika 90 ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Mabao yaliyoipa ushindi Azam FC katika mchezo wa leo yamepachikwa na Himid Mao, Lameck Lawi na Jephte Kitambala huku yale ya Yanga yakiwekwa kimiani na Prince Dube na Bakari Mwamnyeto.

Himid alianza kuifungia Azam katika dakika ya 28 akiunganisha kwa kichwa pasi ya Jean Ngita lakini Yanga ilisawazisha katika dakika ya 67 kwa bao la Dube akiunganisha pia kwa kichwa krosi ya Allan Okello.

Inekuwa ni siku ya mabao ya vichwa kwani, Lameck Lawi aliipatia Azam FC bao la pili katika dakika ya 85 akifunga kwa kichwa mpira wa kona iliyopigwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’

Dakika tatu baadaye, Yanga ikasawazisha kwa bao la kichwa la Bakari Mwamnyeto aliyeunganisha krosi ya Okello na hadi filimbi ya kumaliza dakika 90 inapulizwa, matokeo yalikuwa ni sare ya mabao 2-2.

Ushindi wa Azam FC ulipatikana katika dakika ya 112 kupitia bao la Kitambala aliyefunga kwa kumalizia kwa kichwa mpira uliookolewa vibaya na Ibrahim Abdullah ‘Bacca’.

Azam FC katika fainali, itakutana na Simba ambayo juzi iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Coastal Union.

Mechi hiyo ya fainali itachezwa Julai 4 mwaka huu katika uwanja ambao utatangazwa hapo baadaye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *