Bunda. Shirika la Grumeti Fund limeanzisha programu maalumu ya elimu ya uhifadhi kwa wanafunzi wa shule za msingi katika wilaya za Serengeti na Bunda, hatua inayolenga kujenga kizazi chenye uelewa na ushiriki katika kulinda wanyamapori na mazingira.

Programu hiyo ambayo kwa sasa inatekelezwa katika shule saba za msingi, inawahusisha wanafunzi wa darasa la tano hadi la saba, huku shirika hilo likiwa limeandaa vitabu maalumu vya kusaidia kufikisha elimu hiyo kwa ufanisi.

Akizungumza leo Jumapili Juni 21, 2026 katika maadhimisho ya Siku ya Twiga Duniani yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Kihumbu wilayani Bunda, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Ubunifu (RISE) wa Grumeti Fund, Dk George Lohay amesema elimu hiyo ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi.

Amesema changamoto za uhifadhi zinahitaji suluhisho endelevu, ikiwamo kuwafikia watoto wakiwa wadogo ili kujenga msingi wa kuwa wahifadhi wazuri hapo baadaye.

“Uhifadhi unakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinahitaji ufumbuzi wa kudumu. Njia mojawapo ni kuwaelimisha watoto wakiwa katika umri mdogo ili watakapokuwa waweze kuwa sehemu ya kulinda rasilimali hizi,” amesema.

Dk Lohay amesema programu hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano na walimu wa shule hizo ambao wamepewa mafunzo kuhusu masuala ya uhifadhi ili waweze kuwasaidia wanafunzi kupata uelewa sahihi.

Akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Twiga Duniani, amesema wameamua kuadhimisha siku hiyo kutokana na umuhimu wa mnyama huyo kwa Tanzania, akieleza kuwa mbali na kuwa kivutio cha utalii, twiga pia ni sehemu ya nembo ya taifa.

“Twiga kama walivyo wanyama wengine anakabiliwa na changamoto za uhifadhi, hivyo ni muhimu kuikumbusha jamii umuhimu wa kumlinda na kumtunza,” amesema.

Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Marwa Kitende amesema ujangili na changamoto nyingine za uhifadhi zinaweza kupunguzwa kwa kuongeza uelewa kwa jamii.

Amesema kuwafikia watoto ni hatua muhimu kwa kuwa watakuwa mabalozi wa uhifadhi katika jamii zao.

“Grumeti wamewalenga watoto na ni chaguo zuri kwa sababu itasaidia kuwa na kizazi kijacho chenye uelewa mpana kuhusu madhara ya ujangili na umuhimu wa uhifadhi,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Mahusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori (TAWA) katika mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti, Shija Alex amesema elimu kwa watoto ni njia muhimu ya kuhakikisha kunakuwa na kizazi chenye uelewa wa uhifadhi endelevu.

Ametoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huo kwa kuwa changamoto za uhifadhi zinahitaji ushirikiano wa jamii nzima.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kihumbu wamesema elimu hiyo inapaswa kuendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali ili kila mwananchi awe sehemu ya juhudi za uhifadhi.

Prisca Obugi amesema matamasha na programu kama hizo zinaongeza uelewa kwa wananchi kuhusu faida za utalii na umuhimu wa kulinda rasilimali za nchi.

Naye Nyamhanga Marwa ameomba programu hiyo kufikia shule nyingi zaidi, hasa zilizopo maeneo yanayozunguka hifadhi, ili kujenga jamii yenye ushiriki mkubwa katika uhifadhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *