
Afrika Kusini imesema kuwa itaondoa wanajeshi wake 700 waliokuwa wakihudumu katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO).
Pretoria mwaka jana iliwarejesha nyumbani mamia ya wanajeshi wa nchi hiyo waliokuwua wametumwa Kongo kuhudumu katika kikosi kingine cha askarijeshi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) baada ya wanajeshi wake 17 kuuawa katika mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23.
Taarifa kutoka ofisi ya Rais wa Afrika Kusini imeeleza kuwa Rais Cyril Ramaphosa amemtaarifu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres juu ya uamuzi wa serikali ya Afrika Kusini wa kuondoa mchango wake wa wanajeshi.
Afrika Kusini imechukua uamuzi wa kuondoa wanajeshi wake huko Kongo kufuatia kuwepo haja ya “kuunganisha na kurekebisha rasilimali za Jeshi la Ulinzi waTaifa la Afrika Kusini” baada ya miaka 27 ya kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa za kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Serikali ya Afrika Kusini imesema kuwa suala la kuwarejesha nyumbani wanajeshi wa Afrika Kusini kutoka Kongo nchi ambayo ni miongoni mwa nchi kumi zinazoongoza kwa kuchangia wanajeshi wa kulinda amani katika kikosi cha MONUSCO litakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Mzozo wa mashariki mwa Kongo ulipamba moto mapema mwaka jana baada ya waasi wa M23 kuteka nyara maeneo mengi na miji muhimu ya kimkakati.