Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa ingawa Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kikamilifu kutoa jibu la haraka, kali na litakaloleta majuto kwa uchokozi wowote, haina nia ya kuanzisha vita vya kikanda.

Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi aliyasema hayo Jumapili alipokuwa akihutubia kundi la makamanda na wanajeshi wa Jeshi la Anga na Ulinzi wa Anga la Iran, wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Jeshi la Anga la Iran.

Alisema: “Ingawa walengwa wa vita vya kikanda ni watakaoanzisha uchokozi , vita kama hivyo vitasababisha eneo hili kurudi nyuma kimaendeleo na kimaisha kwa miaka mingi, na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni, kama wachochezi wa vita, watawajibishwa kwa athari zake.”

Jenerali Mousavi amesisitiza kuwa Iran ina uwezo na maandalizi yote muhimu kwa vita vya muda mrefu dhidi ya Marekani.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Tehran bado inakaribisha mianya ya kimantiki ya mazungumzo, mradi isiwekewe masharti yasiyo na msingi wala busara.

Kwa mujibu wa Jenerali Mousavi, taifa la Iran kwa kipindi cha miaka 47 iliyopita limeshuhudia ukatili, usaliti, hila, vitisho, tamaa, njama za kutawala kwa mabavu, pamoja na matamanio yasiyo ya kibinadamu ya Marekani ya “kulimeza” taifa hili.

Alibainisha kuwa: “Mambo yote haya yamekifanya kizazi cha leo kuwa makini zaidi, chenye msimamo, uwezo na azma thabiti ya kusimama kidete dhidi ya adui huyu mwovu.”

Hapo awali, kamanda huyo mkuu alikuwa ameonya kuhusu jibu kali na lenye kuangamiza kutoka Iran dhidi ya vitendo vya uhasama, akisisitiza kuwa jaribio lolote la kulazimisha vita dhidi ya nchi hiyo litashindwa.

Katika ujumbe alioutoa Jumamosi, Jenerali Mousavi alisema kuwa Jeshi la Anga la Iran kwa sasa liko katika kiwango cha juu kabisa cha utayari, na kwa uratibu kamili na matawi mengine ya Majeshi ya Ulinzi, liko tayari kukabiliana na tishio au uchokozi wa aina yoyote kwa jibu thabiti na lenye nguvu.

Jenerali huyo alihitimisha kwa kusisitiza kuwa Iran haitaanzisha vita kamwe, lakini haitasita hata kwa muda mfupi kulinda kwa nguvu usalama wake wa taifa, maslahi yake muhimu na mipaka ya ardhi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *