Mwanachama wa ngazi za juu wa harakati inayotawala nchini Yemen ya Ansarullah ameonya kuhusu uwepo wa vikosi vya jeshi la Israel katika maji ya Somalia, akisema kwamba kupelekwa huko wanajeshi hao kutatambuliwa kuwa shabaha halali.

Mohammed al-Farah, mjumbe wa Idara ya Siasa ya harakati ya Ansarallah, ameonya kuhusu harakati zinazoendelea za utawala wa Israel na Marekani nchini Somalia, akisema: “Tunaitambua Bahari Nyekundu na Lango-Bahari la Bab el-Mandib kama eneo muhimu sana la kimkakati.”

“Harakati yoyote ya adui Mzayuni na Marekani katika eneo hilo itatafsiriwa kama jaribio la adui la kuzidisha ushawishi wake na kudhibiti njia muhimu za majini, na kutishia usalama wa eneo lote, ikiwa ni pamoja na Saudi Arabia yenyewe,” ameongeza Mohammed al-Farah.

Amesema uwepo wa vikosi vya jeshi la Israel katika maji ya Somalia ni tishio kwa usalama wa taifa wa Yemen.

“Sisi nchini Yemen tunaona harakati kama hizo kuwa ni tishio la moja kwa moja kwa usalama na mamlaka ya taifa la Yemen; kwa hivyo, kiongozi wa Ansarullah, Abdul-Malik Badruddin al-Houthi ametoa onyo la wazi na kali kwamba uwepo wowote wa kijeshi wa Israel au Marekani huko Somaliland utatambuliwa kuwa ni tishio la moja kwa moja na utashughulikiwa kwa nguvu,” Farah alisema.

Ameongeza kwamba uwepo wowote kama huo utakuwa shabaha halali na utatambuliwa kuwa ni “mstari mwekundu” ambao haupaswi kuvukwa kwa njia yoyote.

Mwanachama huyo wa ngazi ya juu wa Ansarullah amesisitiza kwamba hakuna haja ya kulinda Bahari Nyekundu kupitia vituo vya kigeni au uwepo wa majeshi ya kigeni katika eneo hilo.

Israel ilitangaza kuitambua Somaliland kama dola huru mnamo Desemba 2025, hatua ambayo Somalia iliipinga na kuilaani vikali, ikiitaja kuwa ni “shambulio la makusudi dhidi ya mamlaka na uhuru wa Somalia.” Aidha nchi za Afrika, Kiarabu na Kiislamu duniani zimepinga vikali hatua ya utawala wa Israel kuanzisha uhusiano na eneo la Somaliland ambalo ni sehemu ya Somalia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *