ARUSHA: SERIKALI imetekeleza jumla ya miradi 81 ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara yenye thamani ya Sh bilioni 500.
Taarifa hiyo iimetolewa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega katika maadhimisho ya siku 100 za mafanikio ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya ujenzi.

Miradi hiyo imehusisha ukarabati wa barabara za lami, ujenzi wa madaraja pamoja na uwekaji wa taa za barabarani katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza katika eneo la King’ori, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Ulega amesema wizara hiyo imepokea jumla ya Sh bilioni 511 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, ambapo Sh bilioni 280 zimetolewa na hazina na Sh bilioni 222 zimetokana na wahisani.
Amesema kati ya fedha zilizotolewa na hazina Sh bilioni 125 zimeelekezwa katika Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi wadogo wanaotekeleza miradi katika maeneo mbalimbali nchini.

“Katika miradi hiyo 81, miradi 40 imekamilika kwa asilimia 100, ikiwemo mradi wa King’ori wa ujenzi wa daraja pamoja na uwekaji wa taa 136 za barabarani, jambo ambalo limeondoa hatari kwa wananchi wakati wa mvua na kuleta tabasamu kwa wakazi wa eneo hilo,”
Aliongeza kuwa uwekaji wa taa za barabarani umechochea shughuli za kiuchumi nyakati za usiku, hususan kwa wafanyabiashara, na hivyo kuchangia kukuza uchumi wa wananchi mmoja mmoja.
Kuhusu uwajibikaji, Waziri Ulega amesema akiwa safarini kutoka Dodoma kukagua miradi ya miundombinu ya barabara, alikuta foleni kubwa ya malori katika eneo la mizani ya Mikese mkoani Morogoro, ambapo baada ya uchunguzi alibaini foleni hiyo ilisababishwa na uzembe wa watendaji.