Timu tatu za kutoka Tanzania kati ya nne juzi zilicheza mechi zake za mzunguko wa tano kwenye mashindano ya Afrika lakini matumaini pekee yamesalia kwa timu mbili ambazo zimebakiza dakika 90 za mwisho kuibeba nchi kwenda robo fainali.
Simba, Yanga zinashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Azam na Singida ambayo ilicheza jana zinashiriki Kombe la Shrikisho ikiwa ni mara ya kwanza Tanzania inafanikiwa kuingiza timu nne kwenye hatua ya makundi ya michuano hii mikubwa, hata hivyo kwa upande wa Simba yenye ilishaaga mashindano hayo hata kabla ya mchezo wa juzi dhidi ya Petro Atletico ya Angola.
Sasa matumaini ya kimahesabu yamebaki kwa timu mbili Azam na Yanga na kama Singida ilifanikiwa kupata ushindi kwenye mchezo wake wa jana dhidi ya CR Belouizdad.
Baadhi ya wachezaji wa Simba, wakipongezana baada ya kupata bao la kusawazisha dhidi ya Petro Atletico katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Picha na Simba
Petro Atletico vs Simba
Simba imemaliza safari yake rasmi juzi licha ya kugomea unyonge baada ya kulazimisha sare ugenini ya kufungana bao 1-1 dhidi ya wenyeji wao Petro Atletico ya Angola tena mnyama akicheza pungufu kwa zaidi ya dakika 50 za mchezo huo baada ya beki wake wa kulia na nahodha wa timu hiyo Shomari Kapombe kupewa kadi mbili za njano mbili zilizozaa nyekundu ndani ya dakika 40 za kwanza.
Kama isingekuwa kadi ile basi pengine Simba ingefanya vizuri zaidi kwani licha ya kutangulia kuruhusu bao mapema dakika ya 13, kisha baadaye kucheza pungufu, wekundu hao walitulia na kuwabana vizuri Petro huku wakicheza soka la mashambulizi ya kushtukiza.
Simba inaendelea kuimarika ambapo ukitazama namna bao lake la kusawazisha wakitumia akili ya kupokonya mpira wakitumia pasi tatu tu kutoka kwa winga Inno Loemba kisha kumpa Anicet Oura ambaye kabla ya kwenda kufunga alimuona Seleman Mwalimu pembeni kisha kwenda kusuburia mpira kati na kumalizia kwa akili kubwa.
Simba ilichelewa kuwaka kwenye mashindano haya kutokana na mabadiliko ya kikosi na hata benchi la ufundi lakini kwa namna ilivyocheza mechi hizi mbili za mwisho kabla ya mchezo wa kufungia makundi wekundu hao wanaonekasna kuimarika taratibu.
Simba imefikisha pointi mbili ambapo jana ilipata pointi ya kwanza ugenini katika mechi zake tatu na sasa itaisubiria nyumbani Stade Malien kwenye mchezo wa mwisho utakaopigwa Februari 15 kukamilisha ratiba kwani haitakuwa na safari yoyote hata ikishinda kwa mabao mengi, lakini rasmi sasa itamaliza ya mwisho kwenye kundi hilo kwa kuwa inaishia pointi tano.
Klabu ya Azam imevuna jumla ya pointi tisa hadi sasa ikiwa inashiriki kwa mara ya kwanza katika Kombe la Shirikisho Afrika. Picha na Azam FC
Azam yaweka rekodi
Azam imeweka rekodi bora ikicheza mechi za kwanza za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuichapa Union Maniema nyumbani kwa bao 1-0 na kufikisha pointi tisa ambazo hakuna timu ambayo kutoka Tanzania imewahi kufikisha iliposhiriki mechi za hatua hii kwa mara ya kwanza.
Ushindi huo wa Azam kwa bao la kichwa la kiungo wake Sadio Kanoute, limelifanya kundi lake kuwa gumu likisubiri mechi za mwisho kuamua nani anakwenda robo fainali ambapo matajiri hao watakuwa wanawania nafasi hizo dhidi ya Wydad Athletic iliyokuwa uwanjani ugenini jana dhidi ya Nairobi United na Maniema ambao wanalingana nao pointi.
Ugumu ni kwamba Azam inatakiwa kusafiri kuwafuata Wydad kwenye mchezo wa mwisho ikihitaji ushindi kama ambavyo Waarabu hao nao watakuwa wanataka lakini pia Maniema nao wakiwa nyumbani dhidi ya kibonde Nairobi United.
Kama Azam itapoteza mchezo wa mwisho itairahisishia kazi Maniema ambao hata kama watapata sare au ushindi, matajiri hao wa Chamazi wataishia hapo na kuziacha Wydad na Maniema zikienda robo fainali.
Azam ikienda robo fainali itakuwa imepiga hatua kubwa lakini hata kama ikikwama ina kitu kikubwa cha kujivunia ambapo ni Singida Black Stars pekee ambayo kama ikishinda mechi zake mbili ule wa jana na ule wa mwisho itaweza kufikisha pointi walizonazo.
Azam inatakiwa kwenda na hatua kubwa nchini Morocco kwenda kulipiza kisasi ikitaka kuweka historia mpya ingawa haitakuwa rahisi kwao kwani Waarabu hao wameshinda mechi zake mbili za ugenini kwenye kundi lao na anayekwenda kumalizia mchezo wa tatu ni wao.
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, akimpita mchezaji wa AS FAR, katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo Yanga ilipoteza 1-0 Februari 7, 2026. Picha na Yanga
Yanga ni ishu ya hesabu
Yanga nao wameahirisha kesi ikijiweka eneo gumu baada ya kupoteza ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco na sasa matumaini pekee ya mabingwa hao wa Tanzania yamesalia kushinda mchezo wao wa mwisho nyumbani huku ikiomba dua mbaya kwa Wamorocco hao wapoteze mchezo wa mwisho ugenini dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Yanga tiketi ilikuwa kwao kama ingeshinda jana lakini ikashindwa kufanya hivyo ambapo hata nafasi zile bora ilikuja kuzitengeneza kipindi cha pili ikipoteza nafasi tatu za wazi ambazo zingeweza kuwapa tiketi ya kwenda robo.
Yanga ilicheza vizuri mchezo huo hasa kwenye ukuta wake, mabeki wake walifanya kazi kubwa wakiongozwa na nahodha wao Bakari Mwamnyeto na wenzake lakini kosa moja la kumsahau beki wa kulia wa FAR Rabat Anas Bach likaharibu hesabu zao.
Yanga ingeweza kuruhusu bao hilo mapema kama FAR Rabat wangekuwa makini kwani dakika ya 55 Anas Bach alikaribia kufunga kama ambavyo alifanya kwa kutumia madhaifu ya wapinzani wake ambapo kiungo wa pembeni wa wageni alikuwa anashindwa kurudi chini kuja kuwasaidia mabeki wa kushoto.
Ukweli ni kwamba kocha Pedro Goncalves atajilaumu kwa kuchelewa kumtoa Pacome Zouzoua ambaye alikuwa amechoka na akikosea hesabu zake nyingi kwenye kujenga mashambulizi ya Yanga, akiwa pia harudi chini kwa wakati kuwasaidia wenzake.
Yanga sasa inatakiwa kuhakikisha inashinda nyumbani tena kwa mabao mawili na kuendelea bila wao kuruhusu bao huku wakiiombea dua mbaya FAR Rabat ipoteze ugenini mbele ya Ahly tena kwa mabao mawili na kuendelea ili tiketi yao iwe hai kwenda robo kama wakishindwa basi litakuwa pigo kwao kwani utakuwa msimu wa pili mfululizo timu hiyo inashindwa kuvuka hatua ya makundi.