Arusha. Serikali imelipa asilimia 95 ya deni la kihistoria la Sh4.46 trilioni lililokuwa linaikabili mifuko ya hifadhi ya jamii nchini, hatua inayoimarisha ukwasi na ufanisi wa mifuko hiyo katika kuhudumia wanachama wake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, amesema hadi sasa Serikali imelipa asilimia 95 ya deni hilo lililorithiwa kutoka kipindi cha kabla ya mwaka 1999.
Akizungumza leo Jumanne, Februari 9, 2026 jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023, Waziri Sangu amesema ulipaji wa deni hilo umeongeza kasi ya ulipaji wa mafao kwa wakati na kuleta utulivu wa kiuchumi kwa wastaafu.
“Hatua hii imeimarisha ukwasi wa mifuko ya hifadhi ya jamii na kuongeza uwezo wake wa kuwahudumia wanachama kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Ameeleza kuwa kulipwa kwa deni hilo ni sehemu ya mchakato wa maboresho ya Sekta ya Kinga ya Jamii ulioanza mwaka 2018, ukiwa na lengo la kutekeleza Ibara ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotaka mamlaka kuweka taratibu za kuwasaidia wananchi wakati wa uzee, maradhi na ulemavu.
Kwa mujibu wa waziri huyo, maboresho hayo yanaakisi dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kulinda haki za msingi za wananchi na kuhakikisha wanapata hifadhi ya kijamii yenye tija na usawa.
Katika hotuba yake, Sangu amesema uzinduzi wa sera mpya ya mwaka 2023 unahitimisha jitihada za muda mrefu za kuunganisha mifumo ya kinga ya jamii ya uchangiaji na ile isiyo ya uchangiaji, hatua itakayowezesha usimamizi jumuishi na madhubuti wa sekta hiyo.
“Sera hii mpya inaiondoa Tanzania katika mfumo wa zamani uliowahudumia walioajiriwa pekee na sasa inaweka msingi wa hifadhi ya jamii jumuishi kwa Watanzania wote,” amesema.
Ametoa shukrani kwa wadau wa maendeleo, wakiwemo Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) na Shirika la Kazi Duniani (ILO), kwa mchango wao wa kitaalamu uliosaidia kupatikana kwa sera hiyo.