Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Evalist iliyopo kata ya Nyarugusu pamoja na Shule ya Sekondari Lwamudasa wilayani Geita wameondokana na adha ya kutembea kwa miguu zaidi ya kilometa tano kwenda na kutoka shuleni, baada ya kukabidhiwa jumla ya baiskeli 100.

Baiskeli hizo zenye thamani ya takribani Shilingi milioni 80 zimetolewa na shirika lisilo la kiserikali la Asante Afrika Tanzania kwa kushirikiana na Mwamba Mine.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo mkoani Geita, mwakilishi wa waandaaji wa mradi alisema walengwa wakuu ni wanafunzi wanaoishi mbali na shule, kwa lengo la kuongeza mahudhurio ya vipindi, kupunguza uchovu wa safari ndefu na hatimaye kuinua kiwango cha elimu katika shule husika.

Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia wanafunzi kufika shuleni kwa wakati, kuongeza muda wa kujisomea na kuboresha matokeo ya kitaaluma, hususan kwa wanafunzi wanaotoka katika maeneo ya pembezoni.

✍ Ester Sumira
Mhariri @claud_jm
#AzamTVUpdates

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *