DAR ES SALAAM: Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dennis Londo, ameielekeza Tume ya Ushindani (FCC) kuongeza juhudi katika kuchochea uzalishaji wa bidhaa za ndani, kuongeza mauzo ya nje ya nchi pamoja na kuimarisha uzalishaji wenye tija, ili kuchangia kukuza uchumi wa taifa.
Naibu Waziri Londo ameyasema hayo Februari 9, jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi za Tume ya Ushindani (FCC), ambapo amesisitiza umuhimu wa taasisi hiyo kulinda masoko ya ndani dhidi ya ushindani usio wa haki, huku ikiendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje.

Ameongeza kuwa FCC ina wajibu wa kuhakikisha mitaji inalindwa, mazingira ya biashara yanaimarishwa na faida za kiuchumi zinaongezeka, kwa lengo la kukuza uchumi shindani na endelevu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, amesema kuwa tume hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia dira ya Taifa, miongozo ya kisera pamoja na usimamizi madhubuti wa sekta binafsi.

Ameeleza kuwa FCC inazingatia sera za ndani na za kimataifa ili kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa lengo la kuimarisha uchumi wa soko unaozingatia ushindani wa haki na kuleta tija kwa maendeleo ya nchi.