Dar es Salaam. Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu Mo Dewji, ameibuka kuhoji hatua iliyofikiwa katika mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo, wakati uongozi wa Simba ukitangaza kurejesha rasmi zoezi la usajili wa wanachama.

Dewji ameuliza swali hilo leo Februari 10, 2026 kupitia ukurasa rasmi wa Instagram wa Simba, akichangia taarifa iliyotolewa na klabu hiyo ikinukuu kauli ya Mwenyekiti wake, Murtaza Mangungu kuhusu urejeshaji wa usajili wa wanachama, jambo lililoibua gumzo miongoni mwa mashabiki.

“Transformation mmefikia wapi?” ameandika Dewji, akirejea mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.

Maoni ya Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu Mo Dewji aliyochapisha katika ukurasa wa Simba leo Jumanne, Februari 10, 2026.

Katika taarifa hiyo, Mangungu amesema Simba imeingia mkataba na kampuni za Mainstream Group na Nexus Pesa kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la usajili na utoaji wa kadi za wanachama, akisisitiza kuwa zoezi hilo litazingatia matakwa ya Katiba ya klabu kuanzia ngazi ya matawi hadi makao makuu.

“Tumeingia mkataba na wenzetu Mainstream Group na Nexus Pesa. Utoaji wa kadi utafata katiba ya Simba kuanzia ngazi ya matawi hadi ngazi ya makao makuu ya klabu. Ni wakati muafaka kwa wanachama hasa ngazi ya matawi na tutaanza usajili wa matawi hivi karibuni,” amenukuliwa Mangungu.

Ameongeza kuwa utoaji wa kadi za wanachama umepangwa kuanza Machi 27, 2026, akieleza kuwa maandalizi yanahusisha taasisi mbalimbali.

“Tumepanga kuanza kutoa kadi tarehe 27,03,2026. Tunafanya hivyo kwa sababu kuna mambo mengi ya kiutendaji na taasisi nyingi zinahusika katika maandalizi ya utoaji wa kadi hizo,” amesema.

Kuibuka kwa Dewji na kuhoji hatua ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Simba kumezua tafsiri mbalimbali, huku kukionekana kuashiria uwepo wa tofauti za mitazamo ndani ya uongozi wa klabu hiyo.

Ikumbukwe kuwa tangu mwaka 2018, Simba haikuendesha zoezi la usajili wa wanachama wapya hadi sasa, ambapo uongozi wake umetangaza kurejesha rasmi zoezi hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *