Dodoma. Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha sekta ya mifugo nchini kwa lengo la kuboresha mbari za mifugo, kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora za ng’ombe, hatua itakayoongeza ubora wa nyama na wingi wa maziwa bora.
Hayo yamesemwa leo Februari 10, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Bashiru Ally alipokuwa akizungumza na watendaji wa wizara hiyo katika kikao cha uwasilishaji wa maendeleo ya Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC).
Amesema serikali inaendelea kuimarisha uzalishaji wa malisho bora kwa kutumia mbinu za kisayansi, ikiwemo kuanzisha na kusimamia mashamba ya malisho ya kisasa, pamoja na kuhimiza ushiriki wa sekta binafsi katika tafiti, uzalishaji wa malisho na mbegu bora za mifugo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Bashiru Ally, akizungumza na watendaji wa Wizara hiyo katika kikao cha uwasilishaji wa Maendeleo ya Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), kilichofanyika katika Ukumbi Ofisi za Makao Makuu ya Wizara hiyo, leo February 10, 2026 Dodoma.
“Tunataka kuwa na maabara ya rufaa ya mifugo kitaifa yenye vifaa, nyenzo na mitambo ya kisasa ya kubaini na kudhibiti magonjwa ya mifugo,” amesema Dk Bashiru.
Aidha, amewataka wataalamu wa mifugo nchini kuzingatia maadili ya taaluma na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili waweze kuwashauri wafugaji kwa uadilifu na kujenga uaminifu katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa NAIC, Dk Dafay Bura, amesema kituo hicho kinaendelea kuboresha mbari za mifugo kwa kuongeza uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa mbegu za kisasa kupitia teknolojia ya uhimilishaji.
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), Dk Dafay Bura, akitoa wasilisho katika Kikao cha uwasilishaji wa Maendeleo ya Kituo hicho, kilichofanyika katika Ukumbi Ofisi za Makao Makuu ya Wizara hiyo, leo February 10, 2026 Dodoma.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, NAIC ilizalisha na kusambaza jumla ya mbegu 49,000 kwa wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Dk Bura ameongeza kuwa juhudi hizo zinaambatana na kuimarisha rasilimali watu kwa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa mifugo na wadau wengine wa sekta hiyo, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na tija katika uzalishaji wa mifugo nchini.