Rais Masoud Pezeshkian amesema kuwa dunia inapasa kuona jinsi mailioni ya wananchi wa Iran walivyomiminika mitaani katika maandamano ya mamilioni ya wananchi kote nchini ili kulinda mapinduzi yao, kutii uongozi wa mfumo, na kutetea thamani na nchi yao ya kujivunia.
Leo, Jumatano, Februari 11 mwaka inaafikia na tarehe 22 mwezi Bahman mwaka 1404 Hijria Shamsia kwa mujibu wa kalenda ya Iran ambayo ni siku ya maadhimisho ya kutimia mwaka wa 47 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Akizungumza mapema leo Jumatano katika hadhara kubwa ya mamilioni ya watu kwenye maadhimisho ya miaka 47 ya Mapinduzi ya Kiislamu katika Uwanja wa Azadi mjini Tehran, Rais Pezeshkian amesema kwamba Februari 11 ni “siku ambayo watu walisimama dhidi ya dhuluma, ukandamizaji, na uonevu.”
Rais Pezeshkian ameashiria malengo ya harakati za mwamko wa taifa la Iran mwaka 1979, na kusema: “Wananchi wa Iran walifanya mapambano ili kusimamisha uadilifu na kuifanya Iran kuwa huru, na waliwadhihirishia walimwengu kwamba Wairani na Waislamu wana uwezo wa kujenga nchi yao kwa nguvu zao, irada, elimu na sanaa zao, na kujijengea heshima na uhuru wao.”

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria namna adui alivyojaribu kusambaratisha mapinduzi machanga ya nchi hii tangu siku ya kwanza ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamuu kwa hatua kama za kuibua migawanyiko na kufanya mapinduzi na kusema: “Marekani na Ulaya zilifanya njama zao zote ili kusambaratisha Mapinduzi yetu lakini ziligonga mwamba. Walitulazimisha vita vya miaka minane. Walimuunga mkono dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein ili kuigawa vipande na kuishinda Iran, hata hivyo vijana wetu walipambana na kuihami nchi, mfumo na Mapinduzi ya Kiislamu kwa ujasiri kwa kusabilia maisha yao.”
Akiendelea na hotuba yake katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais wa Iran amesema: “Hii leo kama mashahidi wetu wangekuwepo tusingekabiliwa na matatizo mengi. Hawakutafuta dunia, ubinafsi, madaraka na umaarufu. Mashahidi wote hawa kuanzia Meja Jenerali Baqeri na Meja Jenerali Salami hadi Shahidi Soleimani, wote walisabilia maisha yao bila kujulikana kwa ajili ya nchi hii na Mapinduzi ya Kiislamu.”
Rais Pezeshkian amesisitiza umuhimu wa kuendezwa umoja na mshikamano wa ndani, na kwamba licha ya vitisho na njama za kutaka kupotosha vijana wa taifa, hakuna njia mbadala ila mshikamano.
“Sasa zaidi ya hapo awali, tunahitaji mwongozo wa busara wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ili kuweka kando matatizo na migawanyiko, kukurubisha pamoja mitazamo tofauti na kuongoza taifa kuelekea kwenye lengo lililo wazi,” amesisitizia Rais Pezeshkian na kusema: Uwepo wa Kiongozi Muadhamu ni nguvu ambayo imeruhusu mfumo na Mapinduzi ya Kiislamu kusonga mbele kwa nguvu licha ya changamoto zote.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwenye Uwanja wa Azadi mjini Tehran, Pezeshkian ameangazia nafasi muhimu ya nchi za kikanda na za Kiislamu katika kuzuia njama za maadui. Amesema “nchi katika eneo hili, moja baada ya nyingine, zinashiriki wasiwasi na misimamo yao nasi kupitia mazungumzo.”