Wazimbabwe wametofautiana kuhusu hatua ya baraza la mawaziri ya kuunga mkono muswada unaokusudia kubadilisha katiba ili kumruhusu Rais Emmerson Mnangagwa mwenye umri wa miaka 83 kubakia madarakani hadi angalau mwaka 2030.

Ingawa mabadiliko hayo bado hayajawasilishwa bungeni yamepingwa vikali na chama chake tawala cha Zanu-PF.

Upande wa upinzani nchini Zimbabwe umeitaja hatua hii  kuwa “mapinduzi ya kikatiba” wakisema mabadiliko hayo yanapasa kutekelezwa kupitia kura ya maoni ya taifa.

Wakili Tendai Biti amesema kuwa mabadliko yaliyopendekezwa ni kinyume cha sheria na yamekiuka katiba.

Ameongeza kuwa: Muhimu zaidi ni kwamba wanataka kuyafanya mabadiliko hayo nje ya kura mbili za maoni. Njia ya kwanza itakuwa ni kuidhinisha kuondolewa kwa kikomo cha muhula, na ya pili kumuidhinisha aliye madarakani afaidike na marekebisho hayo.

Mwananchi wa kawaida wa Zimbabwe kwa jina la Augustine Kaswaurere amesema kuwa: Rais hapasi kusalia maradakani kwa muda mrefu, na ni vyema kuhudumu kwa muda mfupi na kuwapa wengine nafasi.

Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 83, alitarajiwa kuondoka madarakani mwaka 2028 baada ya kumaliza vipindi viwili vya miaka mitano. Lakini muswada huo unalenga kuongeza muda wa utawala wa rais kutoka miaka mitano hadi saba.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa Baraza la Mawaziri jijini Harare siku ya Jumanne, Waziri wa Haki, Sheria na Masuala ya Bunge, Ziyambi Ziyambi, alisema muswada huo utapelekwa kwa Spika wa Bunge na kuchapishwa rasmi katika gazeti la serikali.

Aliongeza kuwa baada ya uchapishaji, wananchi watapata kipindi cha siku 90 kushiriki mashauriano ya umma kabla ya muswada kuwasilishwa kwa majadiliano rasmi ya Bunge.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *