Tume ya Umoja wa Afrika (AU) imekaribisha kutiwa saini kwa kanuni za marejeo ya mfumo wa kusitisha mapigano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na muungano wa waasi wa AFC/M23.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, AU imesema kuwa makubaliano hayo ni hatua muhimu kuelekea kupunguza mapigano katika eneo la mashariki mwa Kongo, ambalo kwa miaka kadhaa limekumbwa na machafuko na mateso kwa raia.

Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahmoud Ali Youssouf, alisema kuwa mkataba huo ni “hatua kubwa ya kujenga imani” kati ya pande zinazohasimiana, na maendeleo chanya yanayolenga kupunguza uhasama na kurejesha amani na usalama mashariki mwa DRC.

AU pia imeishukuru  Qatar na wahusika wengine wa kimataifa kwa kuunga mkono jitihada za amani sambamba na mpango wa upatanisho unaoongozwa na Rais wa Togo, Faure Essozimna Gnassingbé, ambaye ni mpatanishi mkuu wa AU kwa mgogoro wa mashariki mwa Kongo.

Tume hiyo imeongeza kuwa kuanzishwa kwa mfumo wazi na unaokubaliana na pande zote mbili ni muhimu kwa kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano, kujenga uaminifu, na kulinda raia, ikizihimiza pande hizo kutekeleza kikamilifu masharti yaliyokubaliwa.

Kwa miaka mingi, eneo la mashariki mwa Kongo limekuwa uwanja wa mapigano kati ya vikosi vya serikali na makundi kadhaa ya waasi, ikiwemo kundi la M23.

Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa, kundi la M23 linaungwa mkono na Rwanda na kwa sasa linadhibiti maeneo muhimu ya mashariki mwa Kongo, ikiwemo miji mikuu ya Goma na Bukavu, ambayo yalitekwa mapema mwaka 2025.

Serikali za Magharibi zinakosolewa vikali kwa kuchochea vurugu katika mashariki mwa DRC ili kuendeleza uporaji wa madini adimu yanayopatikana katika eneo hilo, ambayo ni muhimu kwa sekta za teknolojia za kisasa kama simu za mkononi, magari ya umeme, na vifaa vya kijeshi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *