Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imevipatia mafunzo maalum vikundi 12 vya utamaduni wilayani Mkalama, mkoani Singida ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kufungua hazina za utalii wa utamaduni katika kanda ya kati.

Mafunzo hayo yamelenga kuviimarisha vikundi hivyo ili viweze kuendesha shughuli zao kwa tija na kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Msimamizi wa Vikundi vya Utalii wa Utamaduni kutoka TTB, George Mwagane, amesema kanda ya kati ina nafasi ya kimkakati katika kukuza utalii wa utamaduni kwa kuwa jamii zake zimeendelea kuhifadhi na kuenzi mila, desturi na tamaduni zao ambapo amebainisha kuwa TTB inalenga kuiunganisha kanda hiyo na maeneo mengine ya utalii nchini.

Mafunzo hayo yamejikita katika maeneo mawili makuu ambayo ni kurasimisha vikundi na kuimarisha uendeshaji wa shughuli zao kwa kufuata taratibu na miongozo rasmi huku Lengo ikiwa ni kuvijengea uwezo wa kiuongozi, kifedha na kiutendaji ili viweze kushindana katika soko la utalii wa ndani na nje ya nchi.

Hatua hiyo ni mwendelezo wa jitihada za TTB za kuibua fursa za kiuchumi kupitia utalii wa utamaduni, huku ikiimarisha uhifadhi wa urithi wa mila na desturi za jamii za kanda ya kati kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *