Shirika la habari la Reuters limenukuu chanzo kimoja na kutangaza kuwa ujumbe wa Marekani unaojumuisha Steve Witkoff na Jared Kushner, utakutana na maafisa wa Iran mjini Geneva, Uswisi siku ya Jumanne wiki hii.

Sambamba na hayo, Reuters imedai kwamba, jeshi la Marekani linajiweka tayari kwa operesheni ya mashumbulio ya kijeshi ya mtawalia na ya wiki kadhaa ambayo yumkini likaanzisha dhidi ya Iran.

Shirika hilo la habari limeongeza kuwa, siku hiyohiyo ya Jumanne ujumbe huo wa Marekani utashiriki baadaye katika mkutano wa pande tatu na wawakilishi wa Russia na Ukraine.

Ikiwanukuu maafisa wawili wa Marekani ambao hawakutajwa majina, Reuters imeripoti kwamba, jeshi la Marekani linajiandaa kutekeleza operesheni ndefu ya kijeshi ya wiki kadhaa dhidi ya Iran, endapo Donald Trump atatoa amri ya kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kufichuliwa kwa taarifa hiyo na maafisa wa Marekani, ambao wameungumza kwa sharti la kutotajwa majina, kunaongeza hatari ya kutofanikiwa diplomasia inayoendelea kufanyika hivi sasa  kati ya Iran na Marekani.

Shirika hilo la habari limemnukuu mmoja wa maafisa hao akisema, katika operesheni ya mashambulizi ya mtawalia, mbali na jeshi la Marekani kulenga miundombinu ya nyuklia, linaweza kulenga pia taasisi za serikali na za kiusalama za Iran.

Kwa kuzingatia maghala ya makombora iliyonayo Iran, wataalamu wanasema, operesheni kama hiyo itawasababishia hatari kubwa zaidi askari wa Marekani, na wakati huohuo mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran, yatazidisha hatari ya kutokea vita na mapigano ya kikanda…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *