
Siku ya jana, Uwanja wa vijana wa Jakaya M. Kikwete (JMK Park) ulijaa burudani, rangi mbalimbali na michezo ya mwisho wiki, huku mamia ya vijana, familia na wadau wakijumuika kusherehekea miaka kumi ya mchango mkubwa kwa jamii kupitia tamasha la 10 Fest.
Hafla hiyo ambayo ilikuwa wazi kwa umma ilitambua hatua muhimu zilizopigwa na JMK Park, kituo ambacho tangu kufunguliwa mwaka 2015 kimewezesha na kuhamasisha zaidi ya vijana na wananchi 300,000.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja Mwandamizi wa Masoko wa Coca-Cola Tanzania, Kabula Nshimo, alilipongeza JMK Park kwa kuwa alama muhimu ya fursa, matumaini na mabadiliko chanya kwa vijana.
“Ninayo furaha kubwa kusherehekea miaka kumi ya mafanikio ya JMK Park. Hiki ni kituo kinachotoa fursa kwa vijana wa kitanzania kukua, kutambua vipaji vyao na kuamini katika mustakabali wao,” alisema.
Maadhimisho hayo yalifanyika kwa ushirikiano na Kampuni ya Coca-Cola, yakionyesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha jamii na kupanua fursa kwa vijana kupitia michezo. Nshimo alisisitiza kuwa Coca-Cola inaamini jamii hunufaika zaidi pale vijana wanapopewa nafasi ya kutambua uwezo wao kamili.
Kwa miaka kadhaa, Coca-Cola imewekeza kwenye programu zinazowawezesha vijana kukuza vipaji vyao kwenye michezo, ubunifu na ujasiriamali. Dira hii inaendana moja kwa moja na dhamira ya JMK Park. Kama taasisi inayotoa huduma kwa jamii kupitia michezo mingi, uwanja huu unatoa mafunzo bila malipo ya michezo na stadi za maisha kwa vijana na watu wazima, yakisimamiwa na wakufunzi waliobobea. Aidha, kituo hiki kimeweka msisitizo kwenye ushirikishwaji kwa kuhakikisha mabinti na watu wenye ulemavu wanapata nafasi sawa, sambamba na mazingira salama kwa vijana kujijengea kujiamini, uongozi na mtindo bora wa maisha.
Tamasha la JMK Park @10 Fest liliendeleza kaulimbiu hiyo kupitia ratiba pana ya shughuli mbalimbali ikijumuisha soka, mpira wa kikapu wa 5×5 na 3×3, mpira wa kikapu kwa walemavu, mazoezi ya asubuhi, dodgeball na burudani ya muziki.
Mkurugenzi wa JMK Park, Mark Sequeira, alieleza kuwa mafanikio ya taasisi hiyo wanayahesabu kama mafanikio ya watazania na dhamira ya taasisi.
“Kwa miaka kumi, JMK Park imekuwa mahali ambapo vijana wanajenga kujiamini, kugundua vipaji vyao na kufurahia michezo.
“Tunaishukuru Coca-Cola kwa ushirikiano wao katika kutufanikisha hatua hii muhimu, na pia kumshukuru mfadhili wetu mwanzilishi, Symbion Power, kwa kutuunga mkono na kuwezesha miaka 10 ya mafanikio.