
Taasisi ya Utafiti ya Royan Research ya Iran imezindua bidhaa sita mpya zilizotengenezwa ndani ya nchi katika nyanja ya tiba ya seli na uhandisi wa tishu, hatua inayoiweka Iran miongoni mwa mataifa yanayozalisha bidhaa za kisasa za tiba zinazojulikana kama Advanced Therapy Medicinal Products (ATMPs).
Timu ya watafiti katika Royan, taasisi inayotoa huduma kamili katika tiba jadidifu (regenerative medicine) na tiba ya seli , imefanikiwa kupata idhini ya udhibiti pamoja na utayari wa kibiashara kwa bidhaa hizo. Hii ina maana kuwa si tu zimekidhi viwango vya kisayansi na usalama, bali pia ziko tayari kuingia sokoni kwa matumizi ya wagonjwa.
ATMPs ni dawa za matumizi ya binadamu zinazotengenezwa kwa msingi wa jeni, tishu au seli. Sekta hii inachukuliwa kuwa moja ya mapinduzi makubwa katika tiba za kisasa, kwani inafungua milango ya matibabu mapya kwa magonjwa sugu, majeraha makubwa na hata saratani zinazokuwa sugu kwa tiba za kawaida.
Mafanikio haya yanatarajiwa kupanua upatikanaji wa tiba za hali ya juu kwa wagonjwa, huku pia yakipunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa tata za kitabibu kutoka nje ya nchi , jambo ambalo ni somo muhimu hata kwa mataifa ya Afrika Mashariki yanayotafuta kujenga uwezo wa ndani wa teknolojia za afya.
Kuingia kwa Iran katika orodha ya mataifa yanayozalisha bidhaa za juu za tiba ya seli hakutaimarisha tu hadhi ya kisayansi ya Jamhuri ya Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi, bali pia kutaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi unaotegemea maarifa (knowledge-based economy), sekta ambayo nchi nyingi zinazoendelea zinaiona kama injini mpya ya ukuaji.
Kwa mujibu wa ripoti ya kimataifa ya hivi karibuni, jumla ya bidhaa 148 za ATMP ziliidhinishwa mwaka 2025 na mashirika 12 ya udhibiti yanayotambuliwa kimataifa. Kati ya hizo, saba zilitoka Iran, mafanikio yaliyoifanya nchi hiyo kupanda kutoka nafasi ya 12 hadi ya 7 duniani katika sekta hii nyeti ya bioteknolojia ya tiba.
Katika mwaka wa kalenda ya Iran 1402 (sawa na Machi 2023 hadi Machi 2024), kulikuwa na bidhaa moja tu yenye leseni katika tiba jadidifu. Hata hivyo, kufikia Machi 2025, idadi hiyo imeongezeka hadi saba , ongezeko linaloonyesha kasi ya uwekezaji na uvumbuzi katika tafiti za seli na jeni.
Bidhaa hizi zinajumuisha tiba za seli, uhandisi wa tishu, pamoja na tiba ya seli za kinga zilizoimarishwa kijeni aina ya CAR-T (Chimeric Antigen Receptor T-cell therapy). Tiba hizi zinatumika kutibu magonjwa mbalimbali kama vile vitiligo, graft-versus-host disease (GVHD), kupooza kwa ubongo (cerebral palsy), majeraha ya moto, vidonda sugu vya miguu kwa wagonjwa wa kisukari, baridi yabisi (arthritis), na saratani ya damu aina ya B-cell acute lymphoblastic leukemia (B-ALL).
Mafanikio haya yanaashiria mwelekeo mpya ambapo mataifa yanayowekeza katika sayansi ya hali ya juu yanaanza kuvuna matunda si tu kitaaluma bali pia kiuchumi, huku baadhi ya bidhaa hizi za kimatibabu zikiwa tayari zina uwezo wa kuuzwa nje ya nchi.