Kutiwa saini Mkataba wa Maelewano wa Islamabad kati ya Iran na Marekani kumevuruga milinganyo anayoipendelea Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni na kuuweka utawala huo katika hali isiyo na mfano wake ya kutengwa kimkakati, kudhoofika kijeshi na mgogoro wa kisiasa; hali ambayo hata vyombo vya habari vya Israel yenyewe vinaitaja kuwa “mbaya sana kwa Israel.”

‘Hali ya sasa ndiyo hali mbaya zaidi inayoweza kutokea kwa Israel, na Netanyahu amekwama katika hali ngumu.’ Hiki ndicho kichwa cha habari cha gazeti la Haaretz lililoandikwa na Amos Harel, mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa gazeti hilo. Baada ya kutiwa saini Mkataba wa Maelewano wa Islamabad baina ya Iran na Marekani, hakuna mhusika mwingine ambaye anajiona kuwa amepata hasara kubwa katika matukio mapya ya eneo kuliko utawala wa Kizayuni. Ripoti za karibuni za gazeti la Haaretz, zilizokusanywa kutoka ndani ya jamii na miundo ya kisiasa ya Israel, zinatoa picha isiyo na mfano wake ya kina cha mgogoro wa kimkakati wa Tel Aviv; mgogoro ambao haukomei tu kwenye uwanja wa vita wa kusini mwa Lebanon, bali pia unajumuisha uhusiano na Marekani, uhalali wa kimataifa, mshikamano wa ndani, na mustakabali wa kisiasa wa Benjamin Netanyahu. Amos Hariel, mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa Haaretz anazungumzia “hali mbaya zaidi inayoweza kutokea kwa Israel”; ambapo jeshi la utawala huo huko kusini mwa Lebanon limenasa kwenye vita vya kuchosha, vifo vya wanajeshi vinaendelea kuongezeka, malengo yaliyotangazwa hayafikiwi, na wakati huo huo pengo kati ya serikali ya Marekani na utawala huo linazidi kuwa kubwa. Tathmini hii ni kukiri wazi mkwamo wa kimkakati wa mradi ambao Netanyahu alikuwa amepanga kuufikia baada ya operesheni ya tarehe 7 Oktoba.

Netanyahu aliamini kwamba operesheni ya Oktoba 7 ilitoa fursa ya kihistoria ya kuunda upya siasa za kijiopolitiki katika eneo; fursa ya kuharibu muqawama wa Wapalestina, kubadilisha uwiano wa nguvu nchini Lebanon, kuiingiza Marekani katika makabiliano ya moja kwa moja na Iran, na hatimaye kupanua utawala wa Israel Asia Magharibi. Lakini matukio ya baada ya uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran tarehe 28 Februari, yamebadilisha hali ya mambo na kuanzisha mkondo tofauti.

Iran haikusambaratika kama walivyopanga, mhimili wa muqawama haukuvunjika, wala matarajio ya Netanyahu hayakufikiwa. Bali kinyume chake, hali halisi mpya imebatilisha mahesabu mengi ya maadui. Kutiwa saini Mkataba wa Maelewano wa Islamabad katika mazingira kama haya kuna maana kubwa zaidi kuliko makubaliano ya pande mbili. Mkataba huu wa Maelewano unaonyesha wazi kuwa Washington, licha ya kauli mbiu zake za kiidiolojia za kuunga mkono Israel kwa hali na mali, lakini hatimaye imelazimika kuweka pembeni suala hilo na kuzingatia maslahi yake makuu kinyume na matakwa ya Tel Aviv.

Utawala wa Donald Trump umefikia hitimisho kwamba kuendelea kwa mvutano wa pande zote na Iran kutaisababishia Marekani gharama zisizoweza kudhibitiwa, kuanzia masoko ya nishati hadi ushindani na China na namna ya kusimamia migogoro ya kimataifa. Kwa mtazamo huu, kumaliza vita na kuanzisha maelewano na Tehran ni hitajio kuu la kimkakati kwa White House kwa sasa. Hapa ndipo utawala wa Kizayuni unajikuta katika hali hatari isiyo ya kawaida.

Kwa upande mmoja, makubaliano yoyote kati ya Iran na Marekani ni kwa madhara ya kimkakati ya Tel Aviv. Uwepo wa kisiasa wa Netanyahu katika miaka iliyopita ulisimama kwenye msingi wa kueneza propaganda bandia za tishio la Iran na dharura ya kukabiliana nalo. Kupungua mvutano kati ya Tehran na Washington bila shaka kutaondoa chombo chake muhimu zaidi cha kukabiliana na suala hilo kisiasa na kiusalama. Katika upande mwingine, utawala wa Kizayuni kutokana na utegemezi wake mkubwa wa kijeshi, kifedha na kidiplomasia kwa Marekani, hauwezi kupinga ipasavyo uamuzi huo wa Washington. Kama gazeti la Haaretz linavyomnukuu J. D. Vance, Makamu wa Rais wa Marekani akisema kuwa Israel italazimika kukaa kimya na kukubali uamuzi wa Marekani kwa sababu utegemezi wake kwa Marekani ni mkubwa mno.

Nyumbani, Netanyahu pia yuko chini ya mashinikizo makubwa kuliko siku za nyuma. Kumalizika vita na Iran bila kutimiza ahadi kubwa alizotoa, kuendelea mashambulizi dhidi ya miji ya kaskazini mwa Lebanon, kuongezeka majeruhi kusini mwa Lebanon na kushindwa kutoa taswira halisi ya ushindi, kumesambaratisha mtaji wake mkuu wa kisiasa. Kura za maoni zinaonyesha kuwa hata sehemu kubwa ya wafuasi wa jadi wa Netanyahu sasa wana shaka kuhusu kuendelea kwake kwenye njia hii. Netanyahu bado anafuatilia ndoto za matukio ya baada ya Oktoba 7, lakini mbinu za kuzifikia hazipo tena. Wakati huo huo, kutengwa kimataifa utawala wa Kizayuni pia kumeingia katika awamu mpya. Haaretz inaonya kwa sauti kubwa isiyo ya kawaida kwamba ulimwengu utashtushwa na kile kilichotokea Gaza na bila shaka utaiwajibisha Israel. Mauaji ya kigaidi, ukiukwaji wa mamlaka za nchi, uharibifu mkubwa na kupuuza sheria za kimataifa haziwezi kuendelea tena bila kulipwa gharama. Mgawanyiko kati ya utawala huo na Umoja wa Ulaya, kuongezeka ukosoaji katika maoni ya watu wa Magharibi na uwezekano wa vikwazo vya kisiasa na hata kijeshi kutoka kwa washirika wake wa karibu ni dalili za mwenendo huu. Ukweli ni kwamba hujuma za kijeshi dhidi ya Iran sio tu kwamba zimeshindwa kubadilisha milingano ya kieneo kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni, bali pia hali jumla imebadilika kwa madhara ya utawala huo ghasibu. Marekani na utawala wa Kizayuni haziwezi tena kunufaika na mazingira yaliyokuwepo kabla ya hujuma hizo. Eneo limeingia katika awamu mpya; awamu ambayo uwezo wa kuzuia wa Iran, uimara wa mhimili wa muqawama, na mapungufu ya nguvu za Marekani, ni mambo ambayo sasa yanaainisha kila kitu katika eneo hili. Mojawapo ya matokeo muhimu zaidi ya matukio ya hivi karibuni ni kwamba Netanyahu sasa amenasa kati ya chaguzi mbili ngumu: ama akubali hali halisi mpya ya mambo inayotawala katika eneo na kuachana na ndoto zake zisizotimia, au aendelee na matukio ambayo yanaweza kuutumbukiza zaidi utawala wa Kizayuni katika kinamasi cha kutengwa kimataifa, mmomonyoko wa kijeshi na mgogoro wa ndani. Ripoti ya Haaretz inaonyesha kwamba hata ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo zenyewe, kuna swali zito ambalo linahoji kwamba je, sasa wakati umefika wa kusahau ndoto za matukio ya baada ya Oktoba 7 au la?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *