Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 3
Kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny aliuawa kwa kutumia sumu inayopatikana katika chura aina ya ‘Dart Frog’ inayopatikana Kusini mwa Marekani, Uingereza na maeneo mengine ya Ulaya.
Sumu aina ya epibatidine ilipatikana katika sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa mwili wa Navalny ambayo ilichangia kufariki kwake katika gereza moja nchini Urusi miaka miwili iliyopita, ofisi ya mambo ya kigeni ya Uingereza ilisema.
Washirika wake walisema Urusi pekee ndio ina ‘uwezo, motisha na nafasi’ ya kutumia sumu hiyo.
Ikulu ya Kremlin imetupilia mbali uchunguzi huo na kuutaja kama ‘kampeni ya kueneza habari’ kulingana na shirika la habari la Tass News.
Sumu hiyo ni nini?
Epibatidine ni sumu inayopatikana kwenye chura aina ya ”dart frog” kulingana na mtaalam wa sumu Jill Johnson.
”Inanguvu mara mia mbili zaidi kushinda Morphine”, aliiambia BBC Idhaa ya Urusi.
Epibatidine hupatikana wa kwa aina ya chura za ‘dart frogs’ na pia inaweza kuzalishwa kwenye maabara.
Chura hao wakiwa wamezuiliwa hawawezi kutoa sumu hiyo, na aidha sumu hiyo haipatikani kwa urahisi nchini Urusi, washirika wa Ulaya walisema katika taarifa yao.
Speshi za Anthony’s poison arrow frog na Phantasmal poison frog, ni aina za vyura ambazo hutoa sumu hiyo kupitia ngozi yao.
Ingawa epibatidine imechunguzwa na kupatikana kuwa inaweza kupunguza maumivu na uvimbe wa mapafu, huwa haitumiki katika matibabu kutokana na sumu iliyonayo.
Sumu ya chura ‘dart frog’ inafanyaaje kazi?
Sumu hii ina nguvu na huathiri mfumo wa neva, kulingana na Johnson.
Husisimua vipokei vya neva, na ikiwa itatumika sahihi, husababisha misuli kutetemeka, kupooza,kifafa, mipigo ya moyo kupungua, matatizo ya kupumua na baadaye kifo cha ghafla.
Alastair Hay, Professa wa sumu na mazingira katika Chuo Kikuu cha Leeds, anasema athari zake ni kushindwa kupumua na ”yeyote anayepewa sumu hiyo hufa kwa kukosa hewa”.
Sumu hiyo kupatikana kwa mwili wa mtu ”kunaashiria kuwa alipewa kimakusudi,” aliongezea.
Upatikanaji wa sumu hii
Sumu ya Epibatidine haipatikani kwa urahisi, na hupatikana katika eneo moja la kijiografia duniani na kwa kiwango kidogo sana, anaelezea Johnson.
Kulingana na taarifa kutoka ofisi ya mambo ya kigeni ya Uingereza, sumu iliyotumika ilikuwa ya Anthony’s poison arrow frog, speshi ambayo inapatikana tu katika mataifa ya Ecuador na Peru.
Vyura hao huzalisha kemikali hiyo kwa kula vyakula sahihi zinazozalisha alkaloids ambazo hufanya sumu ya epibatidine kujikusanya kwenye ngozi.
Iwapo lishe ya vyura hao itabadilika, sumu hiyo ya epibatidine huisha.
“Kupata chura wa porini katika sehemu hiyo, inayokula chakula stahili ya kutengeneza alkaloids, ni vigumu, si rahisi”,alisema Johnson
“Hii ni njia ya kipekee ya kumpa mtu sumu. Kisa kingine cha sumu ya epibatidine ninayo ijua ilikuwa ya maabara na haikuwa na mauti’
Urusi imesema nini?
Maabara za Ulaya zimedhibitisha kuwa Navalny alifariki kutokana na sumu hiyo ya kipekee, washirika hao walisema .
Moscow awali ilikuwa imesema Navalny alifariki kutokana na sababu za kiasili , ila mke wake Yulia Navalnaya, alikuwa akipinga hoja hiyo na kusema mumewe ‘aliuawa’ kwa kupewa sumu.
Ubalozi wa Urusi mjini London ulikanusha madai kuwa Moscow ilihusika na kifo cha Navalny.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Ambia Hirsi