Akifungua kikao cha mwaka 2026 cha Kamati Maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu Kutokomeza Ukoloni, Katibu Mkuu António Guterres amesema ingawa zaidi ya mataifa 100 yamepata uhuru tangu mwaka 1945, mchakato wa kuondoa ukoloni bado haujakamilika.

Ikumbukwe kuwa tangu mwaka 1960 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekuwa linapitisha maazimio ya kutokomeza hali ya nchi kutojitawala ambapo hadi sasa maeneo hayo kwa sasa yanasimamiwa na Uingereza, Marekani na Ufaransa.

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Courtenay Rattray ambaye ni Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu, Guterres ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Bermuda, Guam, Polinesia ya Ufaransa na Sahara Magharibi barani Afrika.

Mambo muhimu matatu

Katibu Mkuu ametaja vipaumbele vitatu vya kunasua maeneo hayo 17 kutoka mtego wa kutawaliwa, nayo ni: mazungumzo jumuishi kati ya maeneo husika na mataifa yanayoyasimamia; ushiriki mkubwa zaidi wa vijana katika kuamua mustakabali wao wa kisiasa; na hatua za haraka za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hasa kwa maeneo ya visiwa vidogo yanayokabiliwa na kupanda kwa kina cha bahari na hali mbaya ya hewa.

Aidha, amegusia madhara ya muda mrefu ya ukoloni, yakiwemo unyonyaji wa kiuchumi na ukosefu wa usawa wa kimfumo, akizihimiza nchi wanachama kuharakisha juhudi za kufanikisha haki ya kweli ya kujitawala.

“Tuendelee kufanya kazi bila kuchoka, na kwa umoja, kuendeleza harakati za kuondoa ukoloni kwa wote,” amehitimisha Katibu Mkuu kwenye hotuba yake.

Marafiki wa Chata ya UN

Waliochangia kwenye mkutano huo kwa kiasi kikubwa wanapigia ‘chepuo’ mamlaka ya Kamati hiyo yazingatiwe kama njia mojawapo ya kutekeleza maazimio kama lile namba 54/91 la mwaka 2000 lililotaka pamoja na mambo mengine kuandaliwa kwa Mpango Kazi wa kuwezesha nchi hizo kujitawala.

Mjumbe kutoka Venezuela, akiwakilisha nchi 24 za Kundi la Marafiki wa kulinda Chata ya Umoja wa Mataifa amesema, “mwezi Novemba mwaka jana tuliandikia barua kamati hii tukitaka kupata maendeleo ya utekelezaji wa jukumu lake kuu la kutokomeza ukoloni.”

Amekumbusha kuwa wakati umefika wa kuondokana na kauli za msisitizo na tuelekee kwenye utekelezaji.

Kauli ya Sierra Leone

Naye mjumbe kutoka Ofisi ya uwakilishi wa Sierra Leone kwenye Umoja wa Mataifa amegusia azimio namba 1514 la Baraza Kuu la kutaka nchi zinazomilikiwa zipatiwe uhuru na kusema  “ujumbe wangu unasalia umejizatiti kuunga mkono juhudu za Umoja wa Mataifa za kutokomeza ukoloni kwa kuwa utokomezaji wa ukoloni  bado ni kipaumbele kikuu cha kazi za shirika.”

Amekumbusha kuwa nchi zinazotawaliwa bado zinaendelea kukabiliwa na changamoto lukuki kama zile za mazingira, uchumi, kijamii, kitamaduni na kisiasa.

“Tunasisitiza umuhimu wa kuheshimu kanuni za Chata ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na maazimio yaliyopitishwa na Baraza Kuu. Wadau wote, zikiwemo nchi zinazotawala maeneo hayo, wakazi wa maeneo na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa lazima kushirikiana kutatua changamoto hizi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *