Tanga. Kufuatia kifo cha mwanamuziki mkongwe Steven Hiza, kilichotokea jana jioni Februari 17,2026, nyumbani kwake Tanga, kiongozi wa kikundi chake kipya cha muziki, Patrick Kamaley amesema msanii huyo atapumzishwa kesho kwenye makaburi ya Goseji.

Steven Hiza ataendelea kukumbukwa kwa kazi zake makini alizotoa enzi za uhai wake ikiwemo wimbo pendwa “Tanzania Yetu Ndiyo Nchi ya Furaha”

Marehemu Steven Hiza akiwa ameshika Tuzo ya heshima ya TMA  ambayo alitunukiwa mwaka 2024

Patrick ameiambia Mwananchi msanii huyo amefariki ghafla nyumbani kwake.

“Amefariki ghafla, Mungu kamtaka. Lakini huwa anasumbuliwa na athma. Alikuwa pia shemeji yangu, mwili upo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti hospitali Bombo,” amesema.

Hata hivyo kwa upande wake mwanamuziki Duncan Ndumbalo amesema walikuwa pamoja siku moja kabla ya umauti wake.

“Jumapili tulikuwa naye mpaka usiku. Tukio limetokea jana jioni, hiyo juzi hakuwa hata anajisikia vibaya kaondoka alikuwa safi. Hivyo vitu ni mipango ya Mungu,” amesema Duncan

Ameeleza siku hiyo ya Jumapili Februari 15,2026 mpaka muziki unamalizika alikuwa mzima wa afya.

“Tulikuwa tunapiga muziki Ngoleme, Sabasaba. Tunaanzaga saa mbili yeye anaingia saa tano usiku, tuliachana saa nane. Yeye akimaliza huwa anaondoka,”amesema 
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *