
Mjumbe wa Ikulu ya White House Steve Witkoff amepongeza leo Jumatano, Februari 18, “maendeleo makubwa” yanayowakilishwa na mazungumzo yanayowaleta pamoja wajumbe wa Urusi na ule wa Ukraine ili kujaribu kupata suluhisho la miaka minne ya mapigano nchini Ukraine.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Wapatanishi wa Ukraine na Urusi wamehitimisha Jumanne mjini Geneva, siku ya kwanza ya mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Marekani huku kukiwa hakuna dalili zozote zinazoashiria kwamba wamefikia hatua kuelekea kuumaliza mzozo mbaya zaidi barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.
“Mafanikio ya Rais Trump katika kuunganisha pande mbili za vita hivi yameleta maendeleo makubwa,” mjumbe huyo amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X baada ya siku ya kwanza ya mazungumzo huko Geneva kati ya wajumbe wa Ukraine na wale wa Urusi chini ya usimamizi wa Marekani.
Marekani imekuwa ikishinikiza kukomeshwa kwa vita hivi vilivyodumu kwa takriban miaka minne, lakini hadi sasa imeshindwa kufanikisha makubaliano kati ya Moscow na Kyiv hasa kuhusu suala muhimu la maeneo ambalo ndilo limekuwa kiini cha tatizo.
Duru mbili za awali za mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine huko Abu Dhabi hazikuzaa matunda yoyote.
Chanzo kimoja kilicho karibu na ujumbe wa Urusi kilieleza kwa sharti la kutotajwa jina kuwa mazungumzo ya hivi karibuni “yalikuwa magumu mno na yalidumu kwa saa sita.”
Siku ya pili na ya mwisho katika duru hii ya mazungumzo inafanyika leo Jumatano.
Hivi karibuni Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema kuwa Trump amekuwa akimshinikiza kuafiki masharti ya makubaliano hayo.