
Hii leo huko Paris nchini Ufaransa yaliko makao makuu ya UNESCO imetolewa ripoti iitwayo “Kuunda upya sera za ubunifu” yenye kurasa 267 zilizochambua takwimu kutoka zaidi ya nchi 120, na kuonesha kuwa mapato ya kidijitali sasa yanachangia asilimia 35 ya kipato cha wabunifu, kutoka asilimia 17 mwaka 2018 hata hivyo, ukuaji huo unaambatana na kuyumba kwa mapato na ongezeko la ukiukwaji wa hakimiliki.
Wabunifu wanaozungumziwa katika ripoti hii ni pamoja na wanamuziki, watayarishaji wa filamu na wasanii wa maudhui ya kidijitali.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ifikapo 2028, mapato ya watunzi wa muziki yanaweza kushuka kwa asilimia 24, huku watayarishaji wa kazi za sauti na picha wakipoteza hadi asilimia 21 ya mapato yao kutokana na ongezeko la maudhui yanayotengenezwa na AI.
Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Khaled El-Enany katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu ripoti hiyo amesema “Ripoti ya UNESCO ya Kuunda Upya sera za ubunifu, ambayo imekuwa kipimo cha kimataifa kwa muda wa muongo mmoja, inatoa wito wa kuimarishwa na kufanywa upya kwa usaidizi kwa wasanii na wataalamu wa masuala ya utamaduni wakati huu ambapo AI na mabadiliko ya kidijitali yanapobadilisha tasnia za ubunifu. Ripoti hii pia imetoa mwongozo wa sera zaidi ya 8,100.”
Kwa wabunifu na watayarishaji wa maudhui, ujumbe ni wazi: kadri AI na majukwaa ya kidijitali yanavyoendelea kukua, ndivyo kunavyohitajika sera madhubuti zaidi kulinda mapato, hakimiliki na uhuru wao wa kujieleza.
Pengo la ujuzi
Eneo jingine lililoangaziwa katika ripoti hiyo ni pengo kubwa la ujuzi wa kidijitali kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea. Asilimia 67 ya watu katika nchi zilizoendelea wana ujuzi wa msingi wa kidijitali, ikilinganishwa na asilimia 28 tu katika nchi zinazoendelea, hali inayoongeza tofauti za kiuchumi kati ya Kaskazini na Kusini.
Ripoti pia inaeleza kuwa biashara ya bidhaa za kitamaduni ilifikia dola bilioni 254 mwaka 2023, lakini nchi zinazoendelea zinachangia zaidi ya asilimia 20 tu ya biashara ya huduma za kitamaduni, hasa katika soko la kidijitali.
UNESCO inaonya pia kuhusu vitisho vinavyoongezeka dhidi ya uhuru wa kisanii, ikibainisha kuwa ni asilimia 61 tu ya nchi zenye mifumo huru ya kufuatilia uhuru huo, huku wasanii katika maeneo yenye migogoro wakiwa kwenye hatari zaidi.
Kupitia Mkataba wa mwaka 2005 wa Kulinda na Kukuza Tofauti za Maonesho ya Kitamaduni, UNESCO imesaidia zaidi ya nchi 100 kuandaa au kuboresha sera za utamaduni, na zaidi ya sera 8,100 zimepitishwa kuimarisha sekta za ubunifu.