
Ugonjwa huu wa kitropiki uliokuwa haupewi kipaumbele, unaosababishwa na kimelea kidogo kinachoitwa mnyoo bapa ambacho huishi ndani ya maji baridi ikiwemo maziwa, mito, na mabwawa, umekuwa mzigo mkubwa na endelevu kwa jamii zinazoishi kando ya ziwa Victoria na maeneo jirani.
Utekelezaji wa mpango huu uliopewa jina la (STEPPS) unaongozwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kwa ufadhili wa Serikali ya Japan ikishirikiana na Muungano wa mashirika ya dawa kwa watoto na Mfuko wa Kimataifa wa teknolojia ya ubunifu katika afya (GHIT).
Dkt. Paul Erasto Kazyoba, ni Mchunguzi Mkuu wa mradi wa STEPPS na Afisa Mkuu wa Utafiti wa NIMR anabainisha ukubwa wa tatizo hili katika maeneo yanayozunguka ziwa, akisema:
“Katika maeneo ya kanda ya ziwa, moja ya changamoto kubwa ni maambukizi ya vimelea, na mengi zaidi ni maambukizi ya ugonjwa wa kichocho. Hapo awali, tulikuwa tukielekeza nguvu zetu kwa watoto wenye umri wamiaka 6 hadi 14. Hata hivyo, kupitia tafiti mbalimbali, ushahidi umeonesha kuwa hata wale wenye umri wa miaka 5 kushuka chini nao pia wanapata maambukizi ya kichocho.”
Kwa muda wa miezi 18 ijayo, mpango huu umepanga kuwafikia zaidi ya watoto 25,000 katika Halmashauri za Wilaya za Itilima, Sengerema, na Kigoma, likiwa ni jaribio la kwanza la aina yake nchini Tanzania.
Dkt. Kazyoba, anaeleza hatua zilizochukuliwa, “tulifanya tathmini ya vituo vya afya ili kubaini ni vituo gani vinapaswa kuhusika katika mfumo huu wa kupima na kutibu. Hawa wahudumu wa afya tunaowapa mafunzo katika vituo hivi, baada ya takribani mwaka mmoja, watakuwa wakufunzi katika mikoa yao na mikoa ya jirani ambayo upanuzi wa upatikanaji wa dawa za kichocho kwa watoto wadogo utafanywa na nchi.”
Rachel Steven, ambaye ni Mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele katika wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, ameelezea furaha yake kwa uwepo wa mpango huo akisema,
“Ninafurahi sana kwa sababu tunaenda kukata ile mizizi ya kichocho tunapoenda kuanza na hawa watoto wadogo.”
Lengo kuu la kuanza kutibu kichocho mapema ni kulinda afya, ukuaji, na maendeleo ya watoto wadogo ambao hapo awali walikuwa hawana dawa maalum ya umri wao hivyo walitumia za watu wazima bila kuwa na kipimo sahihi. Kwa kupambana na ugonjwa huu tangu utotoni, juhudi hizi zinalenga kutafuta ushahidi wa kisayansi utakaosaidia serikali kupanua huduma hii katika mikoa mingine na nchi jirani za ukanda huu.
Mchunguzi Mkuu Mwenza wa mradi wa STEPPS na Afisa Mtafiti Mkuu kutoka NIMR, Jeremiah Kidola, ameshuhudia mafanikio ya kuanza kwa tiba huku akionesha matarajio kuwa kazi hii itakamalika kwa mafanikio makubwa.
“Leo tumeona watoto wawili wamekuja kwenye kituo hiki ambapo wameweza kupata dawa na tumeona ni kweli kabisa kwamba maelekezo na mafundisho waliyopata yamekaa sawa na kwamba tunategemea hii kazi itafanyika kwa ubora na kwa ustadi mkubwa” .
Mpango huu umekuja wakati muafaka ambapo jamii nyingi za wavuvi na wakulima wa kanda ya ziwa zimekuwa zikitaabika na magonjwa haya yaliyosahaulika kwa muda mrefu kama anavyosimulia Martin Joseph, baba wa watoto wawili kutoka kijiji cha Zagayu, Wilayani Itilima mkoani Simiyu anashuhudia
“Watoto wangu walikuwa na tatizo la kuugua kichocho, niliona dalili walikuwa wanakojoa damu, nikachukua hatua ya kutafuta msaada wa madaktari. Leo nimewaleta hapa kutibiwa, tarehe 29 Januari nitawarudisha tena kuja kuwaangalia kama wamepona,” amesimulia.
Dkt. Paul Erasto Kazyoba anahitimisha kwa kueleza matumaini ya wadau, kwamba matokeo ya jaribio hili yatabadilisha kabisa jinsi nchi inavyopambana na kichocho kuanzia ngazi ya familia akisema kwamba, “kile kitakachofanya kazi wakati wa utekelezaji wa mradi wa STEPPS kitasaidia kutoa mwelekeo wa jinsi ya kupanua upatikanaji na ufikishaji wa dawa ya kichocho kwa watoto wadogo (Arpraziquantel) ndani ya nchi na nje ya mipaka,” amehitimisha.
Mbali na kutoa dawa, ili kuhakikisha huduma inawafikia walengwa kwa usahihi, mradi huu umekuwa ukifanya kazi kwa karibu na Shirika la Afya Duniani WHO, Mpango wa teknolojia sahihi katika afya (PATH) na Mpango maalum wa utafiti na mafunzo ya magonjwa ya kitropiki yaliyokuwa hayapewi kipaumbele (TDR). Dawa zinazotumika kwenye majaribio haya zinatolewa na kampuni ya Merck Healthcare ya Ujerumani.