
Arusha. Hali ya simanzi, majonzi na hofu imetanda jijini Arusha kufuatia kuuawa kikatili kwa mfanyabiashara maarufu wa madini, Abdilah Mussa, maarufu ‘Banjoo’ ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa na majeraha makubwa kando ya barabara katika eneo la Bereko, wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
Banjoo ambaye ni mkazi wa Sanawari jijini Arusha, anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana Februari 12, 2026, chini ya jengo la Ngorongoro alipokuwa akitoka mazoezini (gym).
Tangu siku hiyo hakurejea nyumbani, hadi juzi Februari 18, 2026, mwili wake ulipookotwa kando mwa barabara eneo la Bereko, wilayani Kondoa.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa simu leo Alhamisi Februari 19, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Galus Hyera amesema jeshi hilo limepokea taarifa za kifo hicho na linaendelea na uchunguzi.
“Ni kweli tumepokea taarifa hizo na tunaendelea kuzifanyia kazi. Kwa taarifa za awali, mtu huyo amefariki dunia,” amesema.
Mtoto wa marehemu, Mussa Abdilah amesema baba yake aliondoka nyumbani kwenda mazoezini kama ilivyokuwa kawaida yake siku ya Alhamisi, Februari 12, 2026, lakini hakurejea.
“Tulijaribu kumpigia simu mara kadhaa bila mafanikio, jambo lililotutia shaka. Tukaanza kumtafuta kupitia marafiki na ndugu bila mafanikio,” amesema.
Amesema familia iliamua kutoa taarifa za kupotea kwake kupitia vyombo vya habari, ndipo walipopigiwa simu na watu waliowataarifu kuwa kuna mwili umeokotwa kando ya barabara katika eneo la Bereko mkoani Dodoma.
“Baada ya kusafiri kwenda Dodoma kwa ajili ya kuutambua mwili, tulithibitisha kuwa ni baba yetu,” amesema.
Kwa mujibu wa maelezo yake, mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha makubwa ya kipigo, mikono yote ikiwa imevunjwa na macho kutobolewa.
“Ni tukio la kusikitisha sana. Tulikuta mwili wa baba ukiwa umeharibika vibaya ukiwa na majeraha makubwa na mikono yote imevunjwa. Mbaya zaidi, wauaji walimtoboa macho,” amesema kwa huzuni.
Amesema familia haijafahamu chanzo wala wahusika wa mauaji hayo na imeliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliotekeleza tukio hilo na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Hatujui waliohusika na kifo cha baba yetu. Taarifa tulizopewa zinaeleza kuwa alionekana akitoka mazoezini na kuondoka na watu wasiojulikana na hapo ndipo ilipokuwa mwisho wa mawasiliano naye hadi mwili wake ulipopatikana,” amesema.
Ameongeza kuwa familia inahitaji haki itendeke kwa marehemu na wahusika wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa madini jijini Arusha, Jerome Adam amesema tukio hilo limewashtua na kuwatia hofu wafanyabiashara wengi wa jiji hilo, akidai kuwa marehemu hakuwahi kuwa na mgogoro unaojulikana.
“Kwa namna tukio lilivyotekelezwa, linaibua maswali mengi. Ikiwa si sababu za kibiashara, basi huenda ni chuki binafsi. Hata hivyo, si kifo cha kawaida na kimetuogopesha,” amesema.
Ameongeza kuwa wafanyabiashara wa madini na wengine, wanasubiri matokeo ya uchunguzi wa Jeshi la Polisi ili ukweli ubainike na haki itendeke.