Musoma. Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agnes Marwa, ametoa msaada wa vyakula na vifaa vya usafi binafsi kwa wafungwa na mahabusu wa Gereza la Musoma, ikiwa ni sehemu ya kuwafariji na kuwawezesha kutimiza ibada katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma.

Msaada huo unajumuisha vikoi kwa wanawake kujifunika wakati wa kuswali, tende, tambi, sukari, mafuta ya kupikia kwa ajili ya futari, pamoja na sabuni za kufulia na kuogea, nyembe na mahitaji mengine ya msingi.

Aidha, ametoa Sh180,000 kwa ajili ya kununua king’amuzi kitakachowawezesha kufuatilia vipindi vya ibada na mafunzo ya kiroho kwa mujibu wa taratibu za magereza.

Akikabidhi msaada huo leo Februari 19, 2026 mjini Musoma, Marwa amesema ameamua kugusa kundi hilo ili kuwasaidia kutimiza wajibu wa kidini bila vikwazo, akisisitiza kuwa wafungwa na mahabusu bado ni sehemu ya jamii na wanapaswa kuendelea kujaliwa haki zao za msingi za kiimani.

“Ni muhimu viongozi, hasa wa kisiasa, kuwakumbuka wafungwa na mahabusu katika kipindi hiki. Walituhitaji wakati wa kuomba kura, nasi tunapaswa kuwakumbuka wanapokuwa katika mazingira magumu,” amesema Marwa.

New Content Item (4)
New Content Item (4)

Kwa niaba ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mara, Ofisa Magereza Jackson Murya, amelishukuru mbunge huyo kwa msaada huo na kuwataka wadau wengine kuiga mfano huo, akieleza kuwa misaada ya aina hiyo huwatia moyo wafungwa na mahabusu na kuwajengea matumaini ya kurejea kwenye jamii.

“Huu ni moyo wa uzalendo na upendo wa hali ya juu. Wafungwa wanahitaji kuona kuwa jamii inawajali na kuwaunga mkono katika safari yao ya marekebisho,” amesema Murya.

Baadhi ya wakazi wa Musoma wamepongeza hatua hiyo, wakisema wafungwa na mahabusu ni miongoni mwa makundi yanayosahaulika linapokuja suala la misaada. Eva Lameck amesema jamii imezoea kuelekeza misaada kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kulisahau kundi hilo.

Naye Abiud Samwel, aliyewahi kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani, amesema mahitaji magerezani ni mengi hivyo jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kuwatembelea na kuwasaidia wafungwa mara kwa mara.

“Hii pia ni sehemu ya ibada na huruma kwa binadamu wenzetu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *