
Chaneli ya 12 ya televisheni ya utawala wa kizayuni wa Israel imeripoti kuwa, mizozo ndani ya baraza la mawaziri la utawala huo inazidi kuongezeka baada ya mawaziri muhimu kutojumuishwa katika mijadala nyeti kuhusu jinsi ya kutoa mjibizo dhidi ya hatua ya karibuni ya nchi za Magharibi ya kuitambua nchi ya Palestina.
Kwa mujibu wa duru za kisiasa ambazo hazikutajwa zilizonukuliwa na chaneli hiyo, waziri mkuu Benjamin Netanyahu wa utawala wa kizayuni alifanya mkutano wa dharura ambao haukupangwa mapema Jumapil ili kujadili mijibizo unayoweza kutoa utawala huo. Hata hivyo, baadhi ya mawaziri hususan wa usalama wa taifa Itamar Ben Gvir na wa fedha Bezalel Smotrich hawakualikwa kushiriki mkutano huo.
Duru zilizo karibu na Ben Gvir zimemshutumu Netanyahu kwa kujaribu kulainisha matakwa ya Israel kujipa rasmi mamlaka ya utawala kwenye Ukingo wa Magharibi inaoukalia kwa mabavu.
Ben Gvir na washirika wake wanaripotiwa kushinikiza kuchukuliwa msimamo mkali zaidi, ikiwa ni pamoja na kuharakisha hatua za kuudhibiti kikamilifu Ukingo wa Magharibi na kuivunja serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Kinyume chake, Netanyahu anasemekana anatka utolewe mjibizo wenye mlingano ambao utanusuru muungano wake wa kisiasa na kuepusha mivutano zaidi ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa chaneli ya 12 ya Israel, Netanyahu ameripotiwa kusisitiza katika mkutano huo juu ya umuhimu wa kuwepo uratibu kamili baina ya utawala huo wa kizayuni na serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump katika kubuni mjibizo wa kutoa dhidi ya kutambuliwa nchi ya Palestina na mataifa kadhaa ya Magharibi…/