Bunda. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) Mkoa wa Mara imeombwa kufanya uchambuzi kwenye mifumo ya kielektroniki ya utoaji huduma katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vilivyopo mkoani humo, ili kuepuka changamoto za rushwa zinazoweza kutokea.

Ombi hilo limetolewa mjini Bunda leo Alhamisi Februari 19,2026 na wadau wa Takukuru kutoka sekta ya afya kwenye warsha ya uwasilishaji wa matokeo ya uchambuzi wa mfumo wa kielektroniki wa utoaji huduma katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda.

Wakizungumza katika warsha hiyo, washiriki hao wamesema uchambuzi huo ukifanyika utasaidia kubaini upungufu uliopo na kuelekeza yafanyiwe kazi ili kuepuka athari zinazoweza kutokea kutokana na uwepo wa upungufu huo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda, Dk Andrew Masamu amesema kabla ya uchambuzi uliofanywa na Takukuru kwenye hospitali hiyo, ilikuwa ikikusanya wastani wa Sh1.8 milioni kwa siku, lakini hivi sasa makusanyo yameongezeka hadi kufika Sh4 milioni.

Dk Masamu amesema uongozi wa hospitali hiyo uliona kuna uhitaji wa mfumo wao kufanyiwa uchambuzi ili kubaini changamoto zilizopo na baada ya uchambuzi huo, upungufu uliobainika umefanyiwa kazi na hivi sasa kuna mabadiliko chanya hospitalini hapo.

“Unaweza kuona namna tulivyoongeza makusanyo baada ya uchambuzi, hii ina maana kuwa uchambuzi ukifanyika katika vituo vingi huduma zitakuwa bora zaidi ikiwemo kuongeza makusanyo ya vituo husika,” amesema.

Baadhi ya washiriki wa warsha ya Takukuru kuhusu udhibiti wa mianya ya rushwa katika mifumo ya utoaji wa huduma za afya mkoani Mara.  Picha na Beldina Nyakeke

Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mara, Marko Machele amesema vituo vya kutolea huduma za afya vinalenga kutoa huduma bora kwa wananchi na ili huduma hizo ziwe bora ni lazima kuwepo na mapato ya kutosha.

Akiwasilisha matokeo ya uchambuzi huo uliofanyika katika hospitali hiyo Agosti 2025, Ofisa Uchunguzi wa Takukuru, Godwin Midello amesema uchambuzi huo umebaini kuwepo kwa  upungufu mkubwa ambao kwa namna moja ama nyingine ulikuwa ukisababisha utoaji wa huduma kutokuwa wa kuridhisha, huku hospitali hiyo ukipoteza mapato.

Amesema miongoni mwa upungufu uliobainika ni pamoja na uwezo hafifu wa mifumo ya Tehama kudhibiti malipo pamoja na uwezo hafifu wa mfumo huo kudhibiti utolewaji wa misamaha ya matibabu.

“Uchambuzi wetu pamoja na mambo mengine ulibaini upotevu wa zaidi ya Sh71.4 milioni baada ya watu 6,943 kupatiwa misamaha ya huduma bila idhini ya Katibu wa Afya au Mganga Mfawidhi,” amesema.

Midello amesema uchunguzi huo pia umebaini mfumo huo kukosa ufanisi kutokana na kuwa na uwezo hafifu wa kudhibiti utolewaji wa misamaha ya matibabu sambamba na mapato kukusanywa bila kutolewa stakabadhi.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Mohamed Shariff amesema agizo hilo litaanza kufanyiwa kazi mara moja ikiwa ni sehemu ya udhibiti wa rushwa katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.

Amesema udhibiti wa rushwa katika mifumo ya kielektroniki ya utoaji wa huduma za afya unalenga kuboresha huduma za afya ili ziweze kutolewa kwa jamii kwa kiwango bora kama ambavyo Serikali imedhamiria.

“Hapa tunalenga kuzuia upotevu wa mapato kupitia mifumo hii na kuzuia vitendo vya rushwa kabla havijatokea ili huduma ziweze kuwa bora na kukidhi viwango,” amesema.

Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Kaminyoge amewaagiza waganga wakuu wa halmashauri mbili za wilaya hiyo kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinaunganishwa na mifumo ya Tehama ili kuleta tija.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *