Rombo. Serikali ina mpango wa kurejesha biashara ya kuuza viumbe hai, wakiwemo nyani na tumbili, hatua inayolenga kupunguza athari zinazotokana na wingi wa wanyama hao katika maeneo ya makazi ya watu.

Hayo yamebainishwa leo Februari 19, 2026 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji wakati akijibu changamoto za wananchi wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kuhusu tatizo la uvamizi wa wanyama hao kwenye makazi yao, akiwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba inayoendelea mkoani humo.

“Kuliko kuwaua bure, Serikali kupitia Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) ametuelekeza tuifanyie kazi changamoto iliyotokea, turejeshe biashara ile ya viumbe hai ili nyani na tumbili hawa badala ya kuwaua, wauzwe kuongeza mapato na kuondoa changamoto hii kwa wananchi wetu,” amesema Dk Kijaji.

Ameongeza kuwa: “Huko nyuma tulikuwa na viumbe hai wa porini na ilitokea changamoto mwaka 2016, jambo hili likasitishwa, tukapokea maelekezo ya Serikali kwamba tulifanyie kazi sasa. Kwa mfano, changamoto hii inayotokea inatulazimu kuwaua tumbili au nyani wetu na tumeua nyani zaidi 247.”

Dk Kijaji amesema kupitia Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa), wameingiza mapato zaidi ya Sh363.7 milioni.

“Kupitia hifadhi yetu ya Kilimanjaro, sisi kama Taifa tunajivunia sana na tunawapongeza wana-Rombo kwa kuulinda mkoa wetu lakini na hifadhi yetu ya Kilimanjaro. Hifadhi yetu hii ni ya pili kwa kutupatia mapato mengi ndani ya Taifa letu,” amesema Dk Kijaji.

Malalamiko ya wananchi

Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wananchi wilayani humo, Jenesta Tarimo amesema kwa miaka mingi wanakabiliwa na tatizo la wanyama hao ambao wamekuwa wakiharibu mazao yao kila mwaka.

“Mheshimiwa, tunaomba tupate usaidizi wa kuondoa hawa wanyama waharibifu waliosambaa katika maeneo yetu kwani wanafukua mbegu na kula au kukwanyua mazao machanga, tunateseka sana,” amesema mwananchi huyo.

Mwananchi mwingine aliyehudhuria mkutano huo wa Waziri Mkuu, Silvia Tesha amesema kwa miaka mingi wameshindwa kulima kutokana na uharibifu unaosababishwa na wanyama hao.

“Hatuna chakula kutokana na hawa wanyama, wamekuwa ni kero sana kwetu sisi wananchi, hatuwezi kulima wala kufanya chochote kwenye mashamba yetu,” amesema mwananchi huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *